UPATANISHO WA KISARUFI KATIKA KISWAHILI
ALCHERAUS R. MUSHUMBWA, 2018
1.
Maana ya upatanisho wa Kisarufi
Kwa
mujibu wa BAKITA (2015:1107), upatanisho wa kisarufi ni kukubaliana kisarufi
kunakojitokeza kati ya nomino kiima na kitenzi au na kivumishi kunakobainishwa
na viambishi. Kwa mwongozo huo, tunafasili patanisho wa kisarufi kuwa ni kukubaliana
kisarufi kunakojitokeza kati ya nomino kiima na kitenzi; au, na kivumishi
kunakobainishwa na viambishi. Kukubaliana huku huwa kunahusisha nomino mtenda
au mtendwa, kiwakilishi, kivumishi na kitenzi kwenye mpangilio sahihi wa
sentensi za Kiswahili. Hii ina maana kuwa viambishi (awali) vinavyoambikwa kwenye
kivumishi au kitenzi katika sentensi huzingatia aina ya nomino mtenda au
kiwakilishi chake au nomino mtendwa kwa sababu nomino mtenda au mtendwa kwenye
tungo za Kiswahili huwa ndiyo mhusika anayetolewa taarifa katika tungo husika.
Viambishi vya upatanishi wa kisarufi katika Kiswahili sanifu huteuliwa
kulingana na aina na pia kundi (ngeli) la nomino mtenda au mtendwa
inayoarifiwa. Lengo la upatanisho wa kisarufi ni kuleta maana sahihi na yenye
mantiki kwa wazungumzaji.
Utokeaji wa Upatanishi
wa Kisarufi
Upatanishi
wa kisarufi katika tungo za lugha ya Kiswahili hutokea kwenye vipashio
mbalimbali vinavyounda tungo husika kulingana na taratibu za kisarufi (Mhilu na
Masebo, 2010:1-2).
a) Nomino
na Kivumishi (N+V)
Mizizi
ya vivumishi vya Kiswahili huchukua viambishi vya upatanisho kulingana na
nomino inayovumishwa ipo katika kundi lipi kwa kuzingatia umoja na wingi ili
kuleta uafikiano. Kwa mfano:
1. Mtu
mwema (umoja)/ Watu wema (wingi)
Mbwa
mzuri (umoja)/ Mbwa wazuri (wingi)
2.
Kitabu
changu (umoja)/ Vitabu vyangu (wingi)
Kiti
kirefu (umoja)/ Viti virefu (wingi).
b) Nomino
na kitenzi (N+T)
Upatanisho
huu unahusisha nomino mtenda katika tungo pamoja na viambishi awali
vinavyoambikwa kwenye mzizi wa kitenzi ili kuleta ukubalifu wa tungo kimuundo.
Kitenzi (mzizi) hulazimika kuchukua kiambishi awali kinachoendana na nomino
mtenda kwenye tungo ambapo kiambishi hicho hutambulika kulingana na nomino iko
kwenye kundi lipi la majina katika umoja na wingi. Kwa mfano:
1. Uovu
umezidi mtaani kwetu (umoja)/Maovu yamezidi mtaani kwetu
(wingi)
2. Mto
umekauka (umoja)/Mito imekauka (wingi)
c) Nomino,
kivumishi na kitenzi (N+V+T)
Katika
mpangilio huu wa tungo, upatanisho wake huwa ni ukubalifu wa mpangilio sahihi
wa vipashio (nomino mtenda+kivumishi+kitenzi) ambapo kivumishi (mzizi wake), na
kitenzi (mzizi wake) hukubali kuchukua viambishi awali vinavyoitabulisha nomino
mtenda kwenye tungo hiyo. Upatanisho huu nao hufuata utaratibu wa kuzingatia
aina ya nomino na kundi lake inamojumuishwa katika makundi ya majina. Kwa
mfano:
1. (a)
Ukuta ule umebomoka (umoja)/Kuta zile zimebomoka
(wingi)
(b)
Ukuta wangu umebomoka (umoja)/Kuta zangu zimebomoka
(wingi)
(c)
Ukuta mzuri/mrefu umebomoka (umoja)/Kuta nzuri
/ndefu zimebomoka (wingi)
2.
Kucheza
kwake kunachosha.
d) Kitenzi
na nomino mtendwa (T+N-mtendwa)
Hapa
upatanisho hutokea pale kitenzi kinapotangulia jina au nomino ambayo ndiyo huwa
imeathirika na tendo. Kiambishi cha upatanisho wa mtendwa huwa katika kitenzi
na kiambishi hicho huwa ndicho kiwakilishi cha nomino hiyo kwa utaratibu wa kuzingatia
kundi ambalo nomino hiyo imo. Kwa mfano:
1. Umemtuma
Juma dukani? (umoja)/Umewaita watoto wale? (wingi)
2. Ameikata
kamba yangu (umoja/Amezikata kamba zangu (wingi)
e) Kiwakilishi
na Kivumishi (W+V)
Kiwakilishi
ni neno linalochukua nafasi ya nomino au jina katika sentensi. Hivyo, bila
kuwepo nomino basi nafasi yake inachukuliwa na kiwakilishi. Upatanishi wa
kisarufi pia huvikumba viwakilishi vya Kiswahili pale vinapofanya kazi ya
nomino mtenda au mtendwa katika tungo. Kwa hiyo, upatanishi wa kiwalikishi na kivumishi
ni pale kivumishi (mzizi wake) kinapokubali kuchukua kiambishi awali
kinachowakilisha kiwakilishi ili kuleta ukubalifu wa kimuundo kwenye sentensi.
Kwa mfano:
1.
Mimi
mfupi sana (umoja)/Sisi wafupi sana (wingi)
Huyu
mnene kabisa (umoja)/Hawa wanene kabisa (wingi)
2.
Hiki
chembamba (umoja)/Hivi vyembamba (wingi)
Kile
kifupi (umoja)/Vile vifupi (wingi)
f) Kiwakilishi
na kitenzi (W+T)
Kitenzi
kinachoandamana na kiwakilishi kwenye tungo, mzizi wake huambikwa kiambishi
awali kipatanishi kinachoiwakilisha nomino inayowakilishwa na kiwakilishi hicho
ili kuleta uafikiano wa vipashio hivyo kwenye tungo. Ifuatayo ni mifano ya
upatanisho wa kisarufi kati ya Kiwakilishi na Kitenzi:
1. Hili
limeharibika (umoja)/Haya yameharibika (wingi)
Zuri
limeharibika (umoja)/Mazuri yameharibika (wingi)
2. Ule
umekatwa (umoja)/Ile imekatwa (wingi)
g) Kiwakilishi,
kivumishi na kitenzi (W+V+T)
Katika
upatanisho huu, kivumishi na kitenzi vinavyoandamana na kiwakilishi ili kuunda
tungo, hulazimika kupokea viambishi awali vya upatanishi vinavyowakilisha
nomino mtenda inayowakilishwa na kiwakilishi kilicho katika tungo husika ili
kuleta uafikiano au ukubalifu sawia. Kwa mfano:
1.
Langu
lile limepotea (umoja)/Yetu yale yamepotea
(wingi)
2.
Kimoja
kidogo kimenunuliwa (umoja)/Vingi vidogo vimenunuliwa
(wingi)
h) Kitenzi
na kiwakilishi (T+W)
Hapa,
tungo huwa inahusisha kitenzi na kiwakilishi ambapo kitenzi hutangulia
kiwakilishi cha nomino mtendwa. Upatanisho wake huwa ni pale ambapo kitenzi
hubeba kiambishi cha upatanisho wa kisarufi ambacho huiwakilisha nomino mtendwa
inayowakilishwa na kiwakilishi. Kawa hiyo, ili tungo ilete mantiki na ukubalifu
sahihi inabidi kitenzi kikubali kupokea kiambishi cha upatanisho
kinachowakilisha kiwakilishi cha nomino mtendwa. Kwa mfano:
1. Amepigwa
yeye mwenyewe/Wamepigwa wao wenyewe
Nimetumwa mimi/Tumetumwa
sisi
2. Kimenunuliwa
kirefu/Vimenunuliwa virefu
Hadi kufikia hapa, angalau kwa kiasi, dhana ya upatanishi wa kisarufi
katika lugha ya Kiswahili imeelezewa na kupata picha halisi ya jinsi upatanishi
wa kisarufi huchukua nafasi kwenye lugha ya Kiswahili. Aidha, kinachoweza
kuelezwa kwa ufupi ni kwamba kinachoongoza kanuni ya upatanishi wa kisarufi ni
mlengwa mkuu katika tungo – yaani, nomino mtenda au mtendwa kama
ilivyodhihirishwa kwenye ufafanuzi na mifano yake. Kanuni inayoongoza upatanishi
wa kisarufi inasema kuwa “nomino mtenda au mtendwa pamoja na
kiwalikishi chake itawakilishwa katika kivumishi au kitenzi kinachoandamana
nayo kwenye tungo kwa umbo au maumbo (viambishi) yanayoitambulisha nomino hiyo
kulingana na umilikwaji wake kwenye kundi au ngeli za majina.” Kwa
maana hii basi, kinachofanya utambuzi wa kupachika viambishi vitakavyoleta
upatanishi kwenye tungo ni yale maumbo yanayoiwakilisha nomino husika kwenye
ngeli au kundi inamomilikiwa. Kanuni hii hutambuliwa na watumiaji wa lugha ya
Kiswahili kwenye akili zao pale wanapokuwa wanazungumza au kuandika kwa lengo
la kuwasiliana.
MAREJEO
BAKITA,Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK), Dar es
Salaam: Longhorn Publishers Limited,
2015.
Mhilu, Greyson na Masebo J. A, Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha
Tatu, Dar es
Salaam: Nyambari Nyangwine
Publishers, 2010.
Mlyauki, Justa, E. mulashani na D.
Ndilime, KiswahiliKitukuzwe 3,
Malaysia: Pearson
Education Limited, 2009.
0 maoni: