UHUSIANO WA FASIHI NA JAMII KATIKA MITIZAMO YA FASILI ZA FASIHI

UHUSIANO WA FASIHI NA JAMII WAWEZA KUTAZAMWA KWA FASULI YA MITAZAMO IFASILIYO FASIHI

na
ALCHERAUS R. MUSHUMBWA
Mwl, Shule ya Upili Mwang’halanga
Kwimba, Mwanza – Tanzania

       Ikisiri
Fasihi na Jamii ni dhana ambayo imekuwa ikishughulikiwa sana na kwa kina miongoni mwa wanafasihi pamoja na wahakiki wa fasihi. Aidha, kulingana na upeo pamoja na mlango wa kiutafiti wa mtaalamu, dhana hizi zimekuwa zikifasiliwa na kufafanuliwa kwa mielekeo kulingana na mtaalamu husika; zaidi zimekuwa zikifafanuliwa ama kama dhana mbili tofauti ila zenye kujengana; au,  kama dhana moja inayounganishwa kwa dhima. Kutokana na dhana hizi kuwa na umuhimu mkubwa katika taaluma ya fasihi, makala haya yanalenga si kuleta jambo jipya; bali, kuendeleza utamaduni wa kufafanua dhana hizi kwa mlengo tofauti kidogo.
        Kama mada inavyosomeka, makala haya yanajaribu kufafanua uhusiano wa fasihi na jamii kwa mwongozo wa fasili za mitazamo inayotumiwa na wananadharia wa fasihi kufasili dhana ya fasihi. Katika kutimiza azma hiyo, makala haya yameteua mitazamo mikuu mitano ambayo kwayo fasili zake zinaigemeza fasihi moja kwa moja na jamii
Utangulizi
Fasihi kama tunda la juhudi za wanadamu, ambapo tunda hilo hukidhi kiu na hamu ya wanajamii wenyewe, basi haiwezi kwa hakika, kuachwa ikisimama yenyewe bila kuangaliwa chimbuko lake ambalo ni wanadamu. Kama fasihi chimbuko lake ni wanadamu basi wanadamu hao nao wana chimbuko lao nalo ni jamii waishimo. Vivyo hivyo, haiwezi kuhusishwa fasihi na wanadamu bila kuihusisha na jamii kwani jamii ndiyo chimbuko la wanadamu na ndilo vilevile, chimbuko la fasihi. Kwa maana hiyo basi, kuna unasaba wa wazi katika fasihi na jamii. Katika kudhihirisha hilo kwa ufupi, makala haya yanangazia baadhi ya mitazamo ya fasihi iliyoibuliwa na wanafasihi jinsi inavyoweza kusaidia kufasili uhusiano uliopo baina ya dhana za “Fasihi”’ na “Jamii.”  


      1.1 Maana ya Fasihi
Fasihi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali waliojikita kuichunguza, kwa kutaja baadhi yao. Wamitila (2008:13), anaifasili fasihi kuwa ni sanaa inayotumia lugha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja na maisha yake na huathiri, hugusa au huacha athari fulani na hupatikana katika umbo ambalo linatambuliwa na jamii fulani. Simiyu (2011:9), anatoa maana ya fasihi kuwa ni sanaa inayotumia lugha na matendo kuwasilisha ujumbe juu ya maisha ya binadamu. Anahitimisha fasili yake kwa kusema kuwa fasihi hutumia lugha na matendo kama malighafi yake kupitisha ujumbe. Naye, Malenya (2012:40) anasema kwamba fasihi ni sanaa maalum ya matumizi ya lugha inayotoa mafunzo ambayo yanatumiwa kuielekeza jamii.
Katika fasili hizi za wanazuoni zilizorejelewa kwa ufupi; ni kwamba, tunaona kuwa wanasisitiza suala la sanaa (ufundi) kama sifa au kitambulisho cha fasihi.  Pia, wanatuonesha kuwa sanaa hiyo lazima itumie lugha ili kuweza kufikisha kile ilichokibeba. Lakini sanaa hiyo inakuwa na ujumbe (maudhui) ambayo kwayo ndiyo msingi mkubwa. Ujumbe huu ni maalumu kwa ajili ya jamii. Kwa mwongozo huu, tunaweza kuhitimisha kwa kauli moja kuwa, fasihi ni sanaa idhihirikayo kupitia lugha na matendo ya binadamu hasa pale inapotumika kwa dumuni la kufikisha maudhui yake kwa walengwa (hadhira) wanaoishi katika jamii fulani. Tunaposema fasihi tuna maana ya sanaa. Tunaposema sanaa tunalenga picha ya ufundi wa kuwasilisha lengo fulani. Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa maandishi, michoro na uchoraji au uchongaji. Ama sanaa ni zao linalotokana na ufundi huo. Kwa hiyo, ufundi huo ndio tunaoita sanaa, na fasihi ni sanaa kwa sababu huwasilisha mafunzo yake kwa kutumia ufundi huo unaojipambanua kwa mbinu ya lugha ya binadamu.
        1.2 Dhana ya Jamii
Jamii ni msamiati ambao katika maisha ya kila siku tunautumia kuashiria maana fulani; ama, kulingana na muktadha au kwa maana halisi ya kileksia. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya (2004) inafafanua kiduchu maana ya neno “Jamii” kuwa ni mkusanyiko wa watu au vitu. Vilevile, Kamusi ya Kiingereza Oxford Advanced Learner’s Dictionary (2010), inafafanua kuwa Jamii ni watu kwa pamoja, waishio pamoja kwenye ujima; ni ujima fulani wa watu wenye desturi, tabia na sheria za aina moja. Simiyu (2011:20) anasema kuwa Jamii ni kikundi cha watu wanaotumia lugha moja, wana utamaduni mmoja na wanapatikana katika eneo moja la mastakimu. Kwa hiyo, kwa maoni yetu, ni sawa kabisa kufasili Jamii kama mkusanyiko au kundi la watu waliokusanyika sehemu fulani kama kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa, kanda na taifa. Watu hawa huishi kama wamoja, na wenye kufuata utaratibu au kanuni fulani za kimaisha walizojiwekea wao wenyewe. Mkusanyiko huo wa watu unakuwa na utamaduni wake, unaodhihirika katika mila na desturi na mielekeo fulani ya kimaisha.

 “Fasihi na Jamii” kma dhana kuu
Baada ya kupata dondoo fupi kiasi juu ya dhana ‘Fasihi’ na ‘Jamii’ kila moja kivyake, ni vema kuangalia pia juu ya dhana hizi mbili kama dhana moja.
 Madhali, fasihi ni sanaa ya lugha yenye kufikisha ujumbe kwa hadhira: basi wapokeaji wake ni watu ambao ni zao la jamii. Watu ni zao la jamii kwa kuwa jamii ndani yake kuna watu ambao hao huunda jamii. Basi tunaposema fasihi inatumia lugha kufikisha ujumbe kwa hadhira (watu), moja kwa moja tunalenga kuwa fasihi inafikisha maudhui yake kwa wanajamii. Maoni haya ni sahihi kwa msingi wa kuwa ‘fasihi ni jamii na jamii ni fasihi’. Pengine, kauli ya kwamba fasihi ni jamii na jamii ni fasihi yaweza kukanganya kidogo miongoni mwa watu wanaoweza kusikia kauli hii. Ieleweke hakika, tusemapo kuwa fasihi ni jamii na jamii ni fasihi, ina maana ya kwamba bila jamii fasihi haiwezi kuwepo – kwamba, maisha ya fasihi yanategemea uwepo wa jamii. Na kwa maneno mengine ni kuwa, maisha ya jamii ndiyo chanzo cha fasihi. Vilevile ni wazi kuwa jamii ni fasihi kwani hakuna jamii inayoweza kuwepo bila fasihi. Fasihi ni sehemu ya na ni maisha ya jamii husika. Kwa mwelekeo huu, ni wazi ya kuwa wanajamii ndio wanafasihi; na wanafasihi ndio washughulikao na fasihi au kuidhihirisha na kisha kuitumia sanaa hiyo kueleza bayani jamii yao. Katika kuielezea jamii, fasihi hushughulikia kuonesha mambo yote yaliyomo katika jamii na kuifanya jamii itambulike na kuheshimiwa. Hivyo, fasihi na jamii ni kama pande mbili za sarafu moja.  Kutokana na maelezo haya, ndio sababu makala hii imeteua baadhi ya mitazamo inayoweza kudhihirisha uhusiano uliopo baina ya fasihi na jamii. Uhusiano huo ndio msingi wa makala haya kuwa “fasihi na jamii” mbili zinazojenga kitu kimoja nza zikishaungana na kutengeneza kitu kimoja ni vigumu kuzitenganisha. Baadhi ya mitazamo hiyo inayojadiliwa hapa ni: Fasihi ni Hisi, Fasihi ni Kioo cha Jamii, Fasihi ni Mwavuli wa Jamii, na Fasihi ni Zao la Jamii husika na Mielekeo yake ya maisha.
Mitazamo inayofafanua Uhusiano wa Fasihi na Jamii
Kama lilivyo lengo la makala haya kwamba mchango wake ni kuongeza mchango katika kufafanua uhusiano uliopo baina ya fasihi na jamii. Kipengele hili kinajadili kwa kiwango fulani jinsi baadhi ya mitazamo ya kuifasili fasihi iliyoteuliwa kwenye makala haya inavyodokeza bayani uhusiano kati ya fasihi na jamii. Imeteuliwa mitazamo mikuu mitano ambayo kinaganaga ufafanuzi wake unadhihirisha uhusiano wa ndani na nje wa fasihi na jamii.
Fasihi ni Hisi zipatazo Taarifa kuoka katika Jamii
Fasihi imekuwa ikielezwa katika mtazamo wa hisi. Baadhi ya wanazuoni wamedhubutu hata kukosoa kuwa si vema kuiona fasihi ni hisi, hasa wakiegemea zaidi katika fasili ya hisia za kuguswa moyoni. Kwamba, fasihi ni hisia zitokanazo na mguso wa ndani wa moyoni mwa binadamu au mwanafasihi (msanii). Wanaochukulia mtazamo huu katika mawazo hayo, wanakwenda kinyume kabisa na mtazamo huu kwa kusema kwamba si vema kusema kuwa fasihii ni hisi kwa mwelekeo wa mawazo ya kuwa msanii anaamua kufikisha maudhui yake kwa wapokeaji wake baada ya kuguswa na baadhi ya mambo mbalimbali katika jamii. Na hivyo, kutoa maoni kuwa anapoguswa msanii ndipo anapokuja na jambo na kulieleza kwa maandishi au kwa nyimbo, hadithi, na kucheza. Wanaendelea kwenda kinyume kwa kuhoji kwa hoja kwamba kama fasihi ni mguso au hisia za msanii; je inakuwaje baadhi ya wasanii wanaotoa kazi zao za fasihi zaidi ya moja, wanakuwa wameguswa mara ngapi? Mfano; waandishi wa zamani wa fasihi ambao hawapo tena duniani, wameguswa hadi hivi leo? Ukizingatia kazi zao hadi hivi sasa zinafanya vizuri katika jamii. Hayo ndiyo mawazo kinzani juu ya mtazamo wa “fasihi ni hisi.”
      Lakini kwa tafakuri yetu, tunabainisha upungufu wa upande ulioelezwa mwanzo juu ya maoni ya wanaopinga dhana ya kuwa fasihi ni hisi. Kwani, ukosoaji wao unaonekana ni matokeo ya kutowaelewa vizuri washadadizi wa mtazamo huu. Inaonekana sio sahihi kuiangalia fasihi kama hisia-mguso (wanaokosa mtazamo huo wanaiona fasihi kama hisia mguso). Bali, mtazamo huu wa “Fasihi ni Hisi” utazamwe sahihi, na kuutazama sahihi ni kuutazama katika uelewa wa hisi za mwili wa binadamu. Yaani, hisi tano za mwili wa binadamu (macho, pua, ngozi, masikio na ulimi) ndizo nyenzo kuu zimpatiazo msanii taarifa au ufahamu. Kwa sababu hisi hizi humpatia taarifa mwanafasihi/fanani, mtu huyo hufikisha ujumbe wake kwa wapokezi kwa daraja murua ambalo ni lugha. Sengo na Kiango ni wadau wakubwa katika kuupa heko mtazamo huu; wanasema wazi kuwa:
Ikiwa tutasema fasihi ni hisi ni sawa, lakini jibu lenyewe halitoshelezi haja za kazi, athari na thamani ya neno lenyewe na kitu chenyewe kwa jamii. Mtu asikiapo njaa, ama aonapo baridi, si kwamba anatumia macho kwa kuona baridi bali anatumia ‘hisi’ kwa kuchokonoa utashi wa yote ya mawili. Swali: Je hisi hii ni fasihi? Kwa nini isiwe kama fasihi ni hisi? Kwa upande inaweza ikasemekana kwamba hisi ya njaa, baridi, uchovu n.k. ni sawa na ile ya fasihi kuwa vifaa vinavyotumika kuielezea hali ya hisi hizi zote ni vimoja; kwamba mtu hutumia hisi tano za mwili kujiona kwamba yu mwitaji wa chakula. Lugha, ama ishara nyingine ya aina yake inatumika katika kulieleza tatizo la mhusika. Katika ‘fasihi’ pia, hisi tano za mwili hutumika na lugha ndio kielelezo cha matokeo ya hisi hizo (1973:3).
Hivyo basi, ni dhahiri kwamba mtazamo wa Sengo na Kiango unatupa picha halali kuhusu mtazamo unaosema “fasihi ni hisi”, kwamba binadamu hutumia hisi tano kupata taarifa kutoka kwenye jamii yake na kutumia sanaa ya fasihi kuwasilisha taarifa hizo kwa jamii pia. Taarifa hizo zaweza kuwa mbaya, nzuri; ama za kuonya, kutaarifu, kuliwaza, kuelimisha, mtawalia. Jambo tunaloweza kulieleza hapa ni kwamba mtazamo huu uko sahihi na unaleta mantiki, kwani kwa wigo mpana unatupa taswira mwafaka ya ndoa iliopo kati ya fasihi na jamii. Hivi kwamba, unatuonesha kuwa kabla ya kukiwasilisha kwa hadhira kile kinachotakiwa kuwasilishwa kuna kitu kinachokiibua au kukibaini ambacho ni hisi. Hisi hizi zinatupatia taarifa kutoka katika jamii zetu tunamoishi na fasihi inatusaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikishia wanajamii taarifa hizo kwa ufasaha, na hata watu wa jamii nyinginezo vilevile. Kwa hiyo, ni wazi kuwa fasihi ambayo ni sanaa isingekuwepo kama binadamu asingeumbwa na milango ya fahamu ambayo kwa mtazamo huu ni hisi zinazompatia msanii taarifa anazoziwasilisha kwa njia ya fasihi. Mtazamo huu unaweza kuthibitishwa vizuri na msanii wa sinema za kitanzania, Steven Kanumba katika sinema yake inayoitwa Moses ambapo mhusika mkuu anaonesha jinsi hisi zake za ufahamu zilivyoshuhudia mambo katika maisha yake yaliyomfanya atunge kazi hiyo.
Fasihi ni Kioo cha Jamii
Fasihi kama ufundi na mbinu mwafaka za kufikisha ujumbe kwa hadhira; imefananishwa kama kioo cha jamii husika. Katika mtazamo huu, fasihi inakuwa kioo cha jamii kwani inaaksi matendo ya jamii na kuyaonesha kwa umma. Katika kutimiza azma hii, fasihi inapoaksi jamii yoyote ile, wanajamii wanajiona kupitia kioo hicho. Baada ya kuona taswira zao kwenye kioo, watu wanaona mapungufu yao na kuyarekebisha. Hili linaendana sambamba na jamii kujifunza, kuburudika, kuonywa, na kujirekebisha. Kwa sababu jamii inajiona yenyewe katika kioo (fasihi) kupitia taswira iliyoaksiwa; hivyo, jamii inajierkebisha. Kwa kuwa mtu anapotazama kioo huona taswira yake, na baada ya kugundua sura yake hajaiweka sawa, mtu huyo hujirekebisha ili awe sawa sawia. Maneno haya yanaungwa mkono na wataalamu kama Masebo na Nyangwine (2007:1), pale wanaposema kuwa “mtu anaweza akajitazama akaona taswira yake na akajirekebisha.” Vivyo hivyo, jamii husika inaweza kujifahamu kupitia fasihi yake na kujirekebisha.
Mtazamo huu umejaribiwa kukosolewa na baadhi ya waandishi na watafiti wa fasihi. Miongoni mwa wakosoaji ni Lubandanja na wenzake (2016:3) ambapo wanahoji kwamba “kuchukulia fasihi kama kioo siyo sawa kwani kioo hakiwezi kuonyesha sehemu (sura) zote za mwili ama kitu. Je, fasihi haiwezi kuonyesha maisha yote ya jamii?”
      Kama walivyohoji Lubandanja na wenzie juu ya udhaifu wa mtazamo huu, ukweli ni kwamba swali lao linajijibu lenyewe kwani, kama ilivyo kioo kutoweza kuonesha sehemu zote za mwili wa biadamu bali sehemu tu ya sura yake ndivyo ilivyo pia kwa fasihi kuwa haiwezi kamwe kuangazia maisha yote ya jamii bali huangazia baadhi ya mambo ya kimaisha ya jamii husika kulingana na wakati na lengo la msanii. Endapo tutakubali kuwa fasihi inaangazia maisha yote ya jamii kwa pamoja: (i) ni kuidunisha na kuidumaza jamii kuwa haibadiliki na haiendani na mpito wa wakati. Jamii hudumu milele ila katika mabadiliko yanaoyobainishwa na vipindi mbalimbali na mpito wa kimaisha, na mbadiliko haya huibua mifumo mbalimbali ambayo jamii husika hupitia na mifumo hiyo, kila mfumo huibuka na mtindo fulani wa fasihi unaoeleza jamii hiyo katika mfumo iliyomo. (ii) ni sawa na kusema kuwa hakuna haja ya kuendelea kutunga kazi za fasihi kwani zile zilizokwishatungwa zinatosha na kwa kuwa fasihi huangazia maisha yote basi kazi ambazo zimeshatungwa ziliangazia kila kitu katika jamii zetu na hivyo haina haja tena ya wasanii wapya kutunga kazi mpya za fasihi; (iii) kila kazi ya fasihi hushugulikia masuala kadhaa ya kijamii, ambayo kulingana na uwezo na ufahamu wa mtunzi unapofikia juu ya kuyang’amua mambo ya kijamii. Kwa hiyo, ni vigumu fasihi kuangazia mambo yote ya kimaisha ya jamii husika kwa wakati mmoja na kuyamaliza.
     Mbali na hayo, vyovyote iwavyo, mtazamo wa kuifasili fasihi kama kioo cha jamii, ambacho wanajamii husika hujitazama na kujirekebisha kwa yale yasiyofaa na kudumisha yale mazuri, unatupa mwanga wa kuona kuwa jamii inatumia fasihi kama chombo kujitazama na kujikosoa, kujifunza na kuhimarisha yale yaliyo bora. Mathalani kazi za fasihi karibia zote hufanya kazi ya kioo kama ilivyotajwa, miongoni mwa kazi zinazothibitisha ukweli huo ni kama tamthiliya za Kaptula la Marx (1996) yake E. Kezilahabi na Nguzo Mama (1982) ya P. Mhando. Katika kazi ya Kaptula la Marx inaoneshwa jinsi jamii wa wakati huo ilivyokuwa imekengeuka kwa uongozi wa kiongozi waliyekuwa na imani naye tena imani kuu ya aina ya uongozi wake jambo ambalo linasababisha hali ya jamii hiyo katika nyanja zote za jamii kimaendeleo kupwaya kwa sababu ya mfumo wa utwala uliokuwepo jambo ambalo baadae jamii hiyo ilikuja kubadilika na kubadilisha aina ya uongozi wake kutoka katika ujamaa hadi mfumo wa sasa wa demokrasi na soko huria. Kaprula la Mar ni kazi inayokejeli utawala huo. Vilevile, katika tamthiliya ya Nguzo mama msanii anatumia kazi hiyo kuionesha jamii ilivyo na utamaduni mbovu wa kuwakandamiza wanawake na kupendekeza juhudi za ukombozi wa wanawake jambo ambalo kwa sasa limeshika mizizi na jamii zinabadilika. Hivyo, kazi hizi zimetumika kama vioo vya kuaksi uhalisia wa maisha ya jamii na jamii kuchukua hatua za kujirekebisha.
Fasihi ni Mwavuli wa Jamii
Mwavuli ni kifaa kitumikacho kumkinga binadamu dhidi ya jua na mvua. Kumkinga huko ni kumlinda mtu dhidi ya adha za jua na mvua; na kitendo hiki tunaweza kukiita “kutunza/utunzaji”. Aidha, fasihi nayo tunailinganisha na mwavuli, kwani inatekeleza jukumu kama lile la mwavuli. Fasihi na jamii ni mambo yasiyoweza kutenganishwa. Fasihi yoyote ile, iwe ya masimulizi au ya maadishi, inalinda, inakinga na kuitunza jamii. Kwa kuliona hilo kuwa ni jukumu kuu la kazi ya fasihi iwayo yoyote ile, Sengo na Kiango kwa wasaa mwingine wanajitokeza na kusema:
Fasihi ni kama mwavuli umkingao mtu na mvua au jua; mwavuli-fasihi ni ule uhifadhio amali za maisha ya watu wote bila kuchagua wala kubagua tofauti zilizopo.  [. . .] Amali hizo ndizo zijengazo fasihi. Baada ya kujengwa na jamii, fasihi inazihifadhi. Huzifichua na kuzionyesha amali hizo kwa watu ili waone ubora na uovu wa kila kipengele cha maisha kwa mbalimbali: kwa kujadili, kushauri, kuasa, kuusia, kuadibu, kuelimisha (1973: 3).
        Fasihi inauvaa uhusika wa mwavuli kutokana na kuikinga au kuilinda jamii hasa pale inapozihifadhi amali za jamii ili zisiharibiwe na muda mwingine inazionesha wazi kwa watu na kubaini zile zilizo bora na zile zilizopitwa na wakati. Kulingana na mabadiliko ya wakati amali zisizofaa au kupitwa na nyakati zinaachwa na kutupiliwa mbali; pia fasihi inazihifadhi kama kumbukumbu ili vizazi vinavofuata vijifunze na kuchukua tahadhari. Kwa maana hiyo, kutokana na fasihi kuwa kama mwavuli, tunapata kujua mila na desturi nzuri ambazo kabla ya uwepo wetu zilikuwa zikiishi na zile ambazo ni mbaya zilizofanywa na baadhi ya wanajamii na hivyo kutuwezesha kuendelea kudumisha zile mila nzuri na kutupilia mbali na kupiga vita zile mila mbovu. Kutokana na fasihi kubeba jukumu kama la mwavuli la kuikinga na kuilinda jamii dhidhi ya uovu, wanajamii huwa na tahadhari ya kutokufanya mambo mabaya ambavyo ni kinyume na utamaduni wao ili kulinda heshima na utu wa jamii zao. Tuchukulie mfano wa sinema ya The Devil Kingdomambayo maudhui yake ni kuonesha jinsi watu wanavyotumia mbinu zisizofaa za ushirikina ili kujipatia mali na mwisho wa siku wanajikuta wamefanya makosa ya kumhasi Mungu wao na kuamua kumrudia kwa kutubu na kurudi katika hali ya uchaji Mungu. Mfano mwingine ni mfano wa mashairi ya “Uungwana Kitu Mbali na Vita Havitakuvusha” kutoka katika Diwani ya Midulu. Mashairi haya kwa hakika yanaonesha kutetea mila, desturi na utaratibu wa waungwana wa kutetea uungwana na utulivu au ulindaji wa amani ambayo ni mambo mazuri na amali za jamii ya msanii mtunzi wa kazi hizo. Hivyo maudhui yake ni kukemea watu wanaofanya maovu kwa kukiuka mila na desturi pamoja na wale wanaopenda uvunjifu wa amani kwa kuona kuwa vita ndio njia ya kujenga amani.
 Fasihi ni zao la Jamii na Mielekeo yake
Fasihi ni zao la jamii kwa sababu inatokana na jamii, hivi kwamba wanafasihi ni wanajamii wa jamii fulani na yale wayawasilishayo kwa kutumia fasihi chanzo chake ni jamii na huwafikia jamii pia. Pamoja na kuwa ni zao la jamii fulani, fasihi ni lazima iwe au ifuate mwelekeo fulani wa jamii. Fasihi inajidhihirisha kama zao la jamii kwani, fasihi yoyote ile lazima itolewe na jamii au watu wa jamii hiyo. Kwa hiyo, bila jamii hakuna fasihi. Fasihi kama sanaa, na sanaa hiyo imo ndani ya jamii kwa kupitia mahuluti ya msanii anavyopenda kuufikisha ujumbe kwa hadhira yake ambayo ni jamii. Sambamba, fasihi huendana na mielekeo fulanifulani ya kimaisha katika jamii kwa jinsi ambavyo inatakiwa. Ni ndani ya jamii, fasihi haivuki. Na kwa maana hiyo fasihii lazima iwe na mipaka kuhusu maisha ya jamii inapohusika. Mila na desturi za jamii zinaelezwa na fasihi husika. Fasihi humfanya mtu mwingine aijue jamii fulani kwa kupitia fasihi yake. Fasihi inaweza kutazamwa kama kiwakilishi cha jamii inayohusika. Kwa mfano, katika nchi za eneno la Afrika Mashariki kuna jamii ambazo miongoni mwa uatamaduni wao ni kufanya matukio ya kuwakuza vijana – yaani kuonesha kuwa kijana ametoka katika hatua ya utoto sasa kawa kijana na mtu mzima maarufu kama ‘Jando na Unyago.’ Matukio haya hufanywa kwa kuambatanishwa na fasihi inayoelezea utamaduni huo hasa nyimbo za jando na unyago au tohara. Pia, kuna nyimbo za dini za kuabudu na kusifu. Kazi ijulikanayo kama Utu bora Mkulima (1969) ya S. Robert ni mfano wa fasihi inayoonesha kuwa ni matokeo ya jamii ya wakati huo na mielekeo yake chini ya falsafa ya ujamaa na kujitegemea ambapo watu walijengwa kwa msingi wa kilimo vijini. Hizi kazi zote za kifasihi ni fasihi inayotokana na jamii pamoja na kudokeza mielekeo ya jamii hizo. Kwa hiyo, mtu akiifahamu fasihi ya kabila fulani, basi mtu huyu analifahamu kabila kwa kiasi fulani. Atakuwa anajua sera, siasa, utendakazi, desturi na mila za kabila hilo ambapo mambo hayo yote ni mtokeo ya mielekeo ya jamii husika.
 Fasihi ni Kielelezo cha Jamii
Fasihi ni sanaa itumiayo lugha kufikisha maudhui kwa hadhira. Hadhira ndio walengwa wakuu wa kazi yoyote ya fasihi. Hadhira hao huwa ni wanajamii wa jamii fulani na msanii wa kazi ya fasihi naye pia ni mwanajamii wa jamii fulani. Hivyo, msanii huona, husikia, hufikiri na kutafakari kwa kina juu ya mambo katika maisha ya jamii husika. Akisha kuyabaini na kutafakari baadhi ya mambo katika jamii yake au hata jamii nyingine, msanii huyo, huamua kuyabeba katika umbo la sanaa na kisha kuyawasilisha kwa wanajamii wengine ili wapate kuyaona, kuyafikiria, kuyatafakari na kufahamu kipi kinachoendelea. Yale yote yanayokuwa yamebebwa katika kazi ya fasihi; si mengine, bali ni uwakilisho wa sehemu ya uhalisia wa maisha ya jamii hiyo kama: utamaduni – mila na desturi za jamii husika. Pia, kazi hiyo ya fasihi hujaribu kuonesha baadhi ya kaida na miongozo ya kimaisha ya jamii hiyo. Hivyo, katika kutimiza hayo, fasihi inakuwa inakamilisha jumuku la kuwa kielelezo cha jamii husika. Inakuwa ni kielezo cha kijamii kwa kuwa fasihi inawakilisha sehemu ya maisha ya jamii husika na kuwaonesha wengine kuijua jamii hiyo kupitia kazi fulani ya kifasihi. Fasihi, katika hilo inakuwa ni ishara fulani ya kuielezea na kuifasili jamii husika.
       Wataalamu wa fasihi, Wellek na Warren (1949) wakikubaliana na maoni ya De Bonald, wanaiona fasihi kama kielelezo cha jamii. Wanaamba kuwa “uhusiano kati ya fasihi na jamii hujadiliwa kwa kuanza na kauli ya De Bonald kwamba ‘fasihi ni kielelezo cha jamii.’”Aidha, kutokana ukweli huu tunweza kusema kwamba kazi nyingi za fasihi huwa ni vielelezo anuai vya jamii zao kwani hubeba na kuwakilisha sura za jamii hizo. Ipo mifano mingi ya kazi za kifasihi ambazo huwakilisha maisha ya jamii. Senkoro (1987) anadokeza wazi kuwa maendeleo pamoja na vpindi na mifumo mbalimbali amabayo jamii fulani hupitia huelezwa katika kazi mbalimbali za kifasihi. Hivyo, twaweza kusema maisha ya jamii husika, huweza kuelezeka katika kazi ya fasihi ya jamii hiyo na hivyo tunasema bila shaka kuwa fasihi hizo huwa ni vielelezo kwa jamii zinamoibuka. Mathalani, tukichukulia kazi ya riwaya ya Msomi Aliyebinafsishwa (2012) ya N. Nyangwine ni kielelezo cha jamii ya sasa ya utandawazi hasa iliyojikita katika mfumo wa ubepari wa soko huria ambapo dhana ya maendeleo kwa nchi maskini inasadikika kuwa ya kweli kupitia ubinafsishaji ambapo viongozi wa nchi maskini huweka rehani maliasili za mataifa yao kwa mabepari kwa njia ya ubinafsishaji huku awakijinufaisha wao viongozi na wawekezaji-wabinafsishaji na kuwaacha umma ukiteseka kwa umasikini.
Hoja zinazothibitisha Uhusiano wa Fasihi na Jamii toka kwenye Mitazamo ya iliyoelezwa kudokeza Uhusiano huo
Imetanguliwa kuelezwa katika makala haya kuwa fasihi na jamii ni pande mbili za sarafu moja amabazo hukamilisha kitu kimoja chenye maana kamili. Aidha, dhana hii ndiyo inayotupa kiburi cha kueleza kuwa fasihi na jamii ni mambo yasiyoweza kutenganishwa kamwe na hii ni kwa sababu kuwa “fasihi (yoyote ile) huangaliwa kama asasi ya jamii (Simiyu, 2011:20).” Na kama fasili ni asasi ya kijamii basi haiwezi kutenganishwa na jamii na jamii nayo haiwezi kukana asasi yake. Mara baada ya kuona mitazamo minne iliyofafanuliwa vizuri jinsi inavyofasili dhana ya faihi na jamii, mitazamo hiyo inatupa uwezo wa kubaini hoja zinazothibitisha uhusiano uliopo kati ya fasihi na jamii na hivyo kuzifanya kuwa dhana moja. Zifuatazo ni sifa zinazodokeza uhusiano kati ya fasihi na jamii mara baada ya mitazamo tuliyodadavua:
     Kwanza, mwanafasihi au msanii wa fasihi ni zao la jamii. Tunaposema kuwa msanii wa fasihi ni zao la jamii ina maana kuwa msanii mwenyewe anatoka katika jamii na hivyo kama anatoka kwenye jamii basi ni mwanajamii. Na kama ni mwanajamii, kile anachokitunga hukipata kutoka katika jamii kwa kusaidiwa na milango yake ya ufahamu (hisi) na hukielezea kwa wanajamii wenzake ambao maudhui yanayokuwa yamebebwa na kazi yake ya kifasihi huwalenga na kuwahusu wanajamii wenzake. Kwa sababu hiyo basi tunashawishika kusema ya kuwa kwa kuwa fasihi hupatikana kutoka kwenye jamii na wahusika wote ni wana wa jamii basi maudhui yake huilenga jamii husika.
     Pili, kile anachotunga mwanafasihi hukitoa katika mazingira ya jamii fulani ambayo yeye ni mhusika kwa namna moja au nyingine. Kazi yake ya fasihi anayoiumba msanii, hutokana na ufahamu wa msanii mwenyewe juu ya maisha na matukio ya jamii hiyo kutokana na kufahamu miktadha anuai ya jamii hiyo. Maudhui huyaumba kulingana na aina ya mipaka ya muktadha wa jamii anayoitungia kazi hiyo ya fasihi. Kwa mfano, tukirejea kazi zilizotungwa zenye maudhui sambamba na yale ya kipindi cha harakati za kudai uhuru wa Tanganyika zilikuwa zimeumbwa kwa kuzingatia mipaka ya jamii hizo pamoja na kuzungumzia mambo yaliyokuwa yakisumbua jamii hizo hasa suala la ukoloni. Mathalani kazi za Adam Shafi, Kasri ya Mwinyi Fuad (1975) na Vuta n’Kuvute (1999).
     Tatu, uwepo wa fasihi hudokeza na kuwakilisha matabaka yanayopatika katika jamii hiyo. Fasihi huongelea matabaka mbalimbali yanayopatikana kwenye jamii wanapoishi watu na wanajamii wenyewe ndio wamiliki wa matabaka hayo kama tajiri na masikini, wasomi na wasio wasomi, watawala na watawaliwa, watoto na watu wazima, wanawake na wanaume mtawalia. Matakaba hayo ndiyo hujenga jamii, na fasihi itungwayo kuhusu jamii fulani ni lazima idokeze moja wapo ya jozi ya matabaka yaliyotajwa. Msanii hutunga kazi yake ya fasihi akilenga kuwasilisha maudhui yanayogusa tabaka au matabaka fulani yenye mgongano. Kwa kudhihirisha hilo, tamthiliya ya Kinjekitile (1969) ya Hussein inawakilisha jamii ya watu wa tabaka tawaliwa linalopaza sauti zake na kupiga kelele juu ya unyonyaji na ukandamizwaji unaofanywa na tabaka tawala la wakoloni.
     Nne, fasihi ina sifa ya kuiga jamii. Yaani, msanii huiga mambo au matendo yanayofanywa na wanajamii wenzake na kuyawasilisha kwa wanajamii wenzake akionesha uzuri na ubaya wake. Aidha, wasanii wa maigizo na vichekesho huonesha baadhi ya tabia na matendo yanayofanywa na watu katika jamii zao. Kwa mfano, nchini Uganda kuna msanii mmojawapo wa vichekezo maarufu kama Teacher Mpamire (Mwalimu Mpamire) ambaye huwasilisha sanaa yake ya fasihi kwa mtindo wa maigizo kwa kuiga baadhi ya matendo na sifa za wanajamii wa jamii za Afrika Mashariki.
      Kwa kukomea hapa japo si mwisho wa yote, uhusiano wa fasihi na jamii unabainishwa na lugha inayotumika kuwasilisha kazi fulani ya fasihi kwa hadhira wa jamii. Sifa kuu ya fasihi inayoifanya itofautiane na sanaa nyinginezo ni matumizi ya lugha na lugha ni sifa imhusuyo binadamu na si wanyama. Binadamu ni wanajamii, na mwanafasihi ni mwanajamii pia; lugha aitumiayo binadamu huwa ni lugha ya jamii fulani. Kama lugha itumiwayo na binadamu ni lugha ya jamii fulani mwanafasihi naye ni binadamu na ni mwanajamii katika jamii fulani, basi bila shaka msanii huyo hutumia lugha ya jamii fulani kuumba na kuwailisha kazi yake ya kifasihi kwa hadhira wa jamii. Lugha inayotumiwa na jamii au binadamu hulenga kuwasiliana miongoni mwao na lengo kuu la kuwasiliana huwa ni kupata ujumbe maalumu. Kwa mantiki hiyo basi, lugha ya fasihi ni zao la jamii na hivyo, fasihi na jamii huhusiana kupitia lugha miongoni mwa sababu nyinginezo.
Dima ya Tanzu za Fasihi inavyodhihirisha uhusiano wa Fasihi na Jamii
 Fasihi inajitokeza kama sanaa ndani ya matawi yake makuu mawili; yaani, Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi. Matawi haya mawili ndiyo yanayokamilisha utendaji wa fasihi kwa jumla, kupitia tanzu za kila tawi. Aidha, nui mojawapo ya fasihi, ni Fasihi Simulizi. Hii ni fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Fasihi Simulizi inajitokeza kiutendaji kupitia matawi yake madogomadogo (tanzu) ambayo ni Semi, Ushairi, Maigizo na Hadithi. Kila kitawi kina kazi au dhima zake ambazo zinajitokeza kiutendaji zaidi katika jamii.  Fauka ya hayo, Fasihi Andishi ni fasihi inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Vivyo hivyo, nayo inadhihirisha utendaji wake kupitia tanzu zake ambazo ni Riwaya, Tamthiliya, Ushairi na Hadithi fupi. Tawi hili pia lina kazi zisizotofautiana na pacha wake (fasihi simulizi). Hivyo basi, kupitia Riwaya, Tamthiliya, Hadithi, Semi, Ushairi na Maigizo, fasihi hudhihirisha utendaji wake katika jamii husika. Kila kifani cha fasihi hutungwa kwa ajili ya jamii na huwasilishwa kwa njia ya lugha: ya mazungumzo au maandishi.
      Fasihi na jamii ni mambo ambavyo kuyatenganisha ni kuua mojawapo. Hii ni kwa kuwa mambo haya yanategemeana na kukamilishana. Bila fasihi, sio rahisi kuielewa jamii husika, na bila jamii sio rahisi kuilewa fasihi. Fasihi inatokana na watu waliomo katika jamii, pasipo na jamii hakuna watu. Kwa kuwa sanaa ya fasihi inatoka ndani ya wanajamii ambamo fasihi hiyo inachimbuka, ni mwelekeo sahihi wa mawazo kusema fasihi ina dhima katika jamii kwa jumla; kwa maana hiyo tunaangalia dhima za fasihi.  Fasihi ina dhima au kazi nyingi katika jamii ambazo wanajamii huzikubali na kuziishi. Dhima za fasihi katika makala haya zinatengwa katika mitizamo mikuu miwili ambayo ni Kuelimisha na Kuburudisha.
      Kwa kuanza na kueliemisha, fasihi inalo jukumu la kuwaelimisha wanajamii wake. Ili kukamilisha jukumu hili, fasihi inaonya, inarekebisha, inafahamisha, inatoa mawaidha nakadhalika. Aidha, fasihi uhifadhi amali za jamii. Jamii yoyote ile ina fasihi ambayo hushughulika na maisha ya jamii hiyo. Shughuli za kiutamaduni na mielekeo ya jamii. Mathalani, nyimbo za Jando na Unyago, tamthiliya ya ‘Kwenye ukingo wa Thim (1988)’. Hizi ni baadhi ya kazi za fasihi ambazo zinaeleza na kuenzi utamaduni wa jamii za Afrika Mashariki na kupitia kazi hizi na nyinginezo nyingi wanaafrika mashariki hujifunza mambo mengi juu ya maisha yao. Aghalabu, fasihi hukuza na kuendeleza lugha ya jamii pia. Hii ni moja wapo ya kazi za fasihi, kwani fasihi hutumia lugha ama maneno ya binadamu kufikisha maudhui katika wapokezi wake. Nyimbo za makabila zimechangia sana kukuza na kuongeza msamiati katika lugha ya Kiswahili, na lugha za makabila, mtawalia. Pengine maghani, nyimbo majigambo, mashairi, ngonjera, vichekesho, soga, methali, vitendawili, miviga nakadhalika; kwa pamoja vipera hivi vya fasihi vimechangia kwa kiasi kikubwa wanajamii kuelewa na kuzoea lugha yao.
      Kadhalika, fasihi inatoa mafunzo na maadili mbalimbali kwa kuonya, kusifu au kukashifu mambo katika jamii. Wimbo wa msanii Saida Karoli, ujulikanao kama ‘Kaisiki’, ni mfano bora unaodhihirisha kuonya, kukosoa, kukashifu na kukejeli baadhi ya mambo mabaya yanayotendwa katika jamii. Wimbo huu unawaonya vijana wa kike na wa kiume wanaoshirikiana na mabinti kutoa mimba. Pia, unakejeli na kukashifu kitendo cha watu kutuma watoto wa wengine, ilhali wao waliwakataa hata kutoa mimba zao. Mfano, baadhi mishororo katika wimbo huu inasema:
                                  Ubeti mmojawapo katika wimbo wa Saida Karoli: ‘KAISIKI’
Mhh…! Toina maani toina mwana, olaba wowaaaa?
Leba wazeea, omugongo gw’ainamileeee!
Owange otakutuma kaisiki iwe…. Owawe okanagagaaaa x2”
Owange otumile no’mubwankya…owange otumileeee,
Owange otumile no’mubwaigoro… owange otumileeee,
Owawe agirea Merisa, owaewe agireaaa?
Tafsiri:
Mhh…! Huna nguvu huna mtoto, utakuwa wa nani?
Ona umezeeka, mgongo umepinda!
Wa kwangu usitume we mama/msichana…wakwako umemtupa x2”
Wa kwangu umatuma hata asubuhi…wa kwangu unatuma,
Wa kwangu unatuma hata jioni…wa kwangu unatuma,
Wa kwako ameenda wapi Merisa, wa kwako ameenda wapi?
 Zaidi ya hayo, katika kutoa elimu, fasihi inaeneza na kuchochea ushirikiano katika jamii. Mfano mzuri ni tamthiliya ya Harusi (1993). Hii ni tamthiliya ambayo inahimiza na kueleza ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki (Kenya na Tanzania). Uhusiano huu si mwingine bali ni wa wanajamii.
      Mwendelezo wa kazi ya fasihi katika jamii unakomea katika dhima ya kutoa burudani kwa wanajamii. Fasihi ni sanaa itumiayo lugha iliyoumbwa kiufundi (fani) kufikisha ujumbe kwa hadhira. Katika fani, fasihi huwasilisha ujumbe kwa njia ya nyimbo, mashairi hadithi, maigizo na mbinu nyingine nyingi kulingana na matakwa ya mtunzi. Katika fani hii, jamii au wapokeaji wa fasihi huburudika pia kwa kufurahi sana, kucheka, na kuchangamsha bongo. Mathalani vitabu vya riwaya pendwa, kama za Erick Shigongo, hadithi za kimahaba, tamthiliya za kwenye runinga na vichekesho vinavyofanywa na wasanii kama vikundi vya “Orijino Komedi – TBC1, Ze Comedy – EATV na Futuhi – Star TV”. Hii ni badhi tu ya kazi za kifasihi zinazofanya kazi ya kuburudisha wanajamii wanaozipokea kazi hizo. Kimsingi dhana ya kuonesha dhima za fasihi katika jamii ni kudhihirisha unasaba uliopo baina ya fasihi na jamii kwa mantiki ya kwamba mitazamo inayoifasili fasihi na jamii ukweli wake unaoneshwa bayani na kazi za fasihi katika jamii.



Hitimisho
Kwa kuhitimisha inaweza kusemwa kuwa fasihi itazamwe kama kiwakilishi cha jamii inayohusikaambamo fasihi yenyewe imetokea. Hivyo, fasihi na jamii ni kitu kimoja - yaani ni sawa na sarafu inayokamilishwa na pande mbili au mtu ambaye anakamilika kwa mwili na roho vinapoungana. Kwa mantiki ya kuwa, pasipo jamii hakuna fasihi na hakuna jamii bila fasihi. Kila jamii lazima iwe na fasihi ambayo ndio kitambulisho chake. Dhana ya fasihi inajieleza maridadi hasa pale inapoangaliwa zaidi kwa kuihusisha na jamii. Jamii haiwezi abadani kujitenga na fasihi yake na fasihi haiwezi kuwa sanaa iliyokamilika kwa kujitenga na jamii; na kama itakuwa hivyo, hakika haitakuwa ni fasihi. Hii ni kwa sababu kwamba fasihi pamoja na kuwa ni miongoni mwa mazao ya jamii, pia ni “taasisi ya kijami; kwani tunaweza kusema kuwa kwani mara nyingi fasihi hutokana na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za kijamii. Taasisi za kiuchumi, kisiasa, na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na utoaji wa fasihi na kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyengine, hudhihiri uweli huu (Ntarangwi, 2004: 21).”
Kama iliyodokezwa kwenye ikisiri, makala hii imechambu na kuchukua baadhi ya mitazamo ambayo kimsingi ufasili wake wa fasihi unaweza kusaidia kuifasili dhana ya uhusiano uliopo kati ya fasihi na jamii.

MAREJEO
Bukagile, G.R & Ngambeki, J. 2005. Kiswahili Kwa Shule za Sekondari. Dar es Salaam:
                  General Booksellers Ltd.
Hornby, A.S. 2010. Oxford Advanced Learners’s Dictionary. 8th Edition. New York: Oxford
             University Press.
Hussein, E. 1969. Kinjekitile. Nairobi: Oford University Press.
Hussein, E. 1988. Kwenye Ukingo wa Thim.Nairobi: Oford University Press.
Kanumba, S. 2011. Devil Kingdom (sinema). Dar es Salaam: The Great Films.
Kanumba, S. 2011. Moses (sinema). Dar es Salaam: The Great Films.
Karoli, S. 2000. ‘Kaisiki.’ Chambua kama karanga. Mwanza: Tivol Studio.
Kezilahabi, E. 1996. Kaptula la Marx. Dar es Salaam: Dar es salaam University Press.
Lubandanja, E.E.N, Robert, P & Sheltiely, D.D. 2016. Kito cha Fasihi: Kwa shule za Upili,
                  Vyuo vya kati na Ndaki. Geita: Lubandanjas’ Junior Publishers.
Malenya, M. M. 2012. Matumizi ya Lugha katika Fasihi Simulizi. Mwanza: Inland Press.
Masebo, J.A & Nyangwine, N. 2007.  Nadharia ya Fasihi. Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine
               Publishers.
Muhando, P. 1982. Nguzo Mama. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Ntarangwi, M.2004. Uhakiki wa Kazi za Fsihi. Augustana College, Rock Island, IL 61201 Nyangwine, N.C.M 2012. Msomi Aliyebinafsishwa. Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine
                   Publishers.
Robert, S. 1969. Utu bora Mkulima.Nairobi: Evans Brothers.
Sayari, A.J. 1993. Harusi. Dar es Salaam University Press.
Sengo T.S.Y & Kiango.D. 1973. Hisia Zetu Na1: Fasihi. Dar es Salaam: Institute of Swahili
                 Research University of Dar es Salaam.
Sengo, T.S.Y.M. 2015. Diwani ya Midulu. Toleo la pili. Dar es Salaam: AKADEMIYA
Senkoro, F.E.M.K. 1987. Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Shafi, A.S. 1999. Vuta n’Kuvute. Dar es salaam: Mkuki na Nyota Publishers.
Shafi, A. S.1975. Kasri ya Mwinyi Fuad. Dar es Salaam:
Simiyu, W F. 2011.  Kitovu cha Fasihi Simulizi. Mwanza: Serengeti Bookshop.
 Taasisi ya Ukuzajia Mitaala Tanzania, 1992. Kiswahili Vyuoni. Dar es Salaam: KIUTA.
TUKI, 2004.  Kamusi ya Kaiswahili Sanifu. Toleo la Pili. Kenya: Oxford University Press.
Wamitila, K. W. 2008. Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Publications.

0 maoni:

Copyright © 2012 JUKWAA LA KISWAHILI - Blogger Theme by SoraTemplates