DHANA
YA SARUFI YA KISWAHILI
na
Alcheraus
R. Mushumbwa, 2017
Maana ya Sarufi
Lugha
za binadamu huwa na mpangilio maalumu wa sauti za binadamu zilizokubaliwa na
wanajamii fulani ili zitumike katika mawasiliano yao - wao kwa wao, kwa kufuata
utaratibu maalumu. Dhana ya lugha kwa jumla inajidhihirisha bayanikatika
mhimili wa mawasiliano; kwa maana kuwa, lugha ni chombo cha kimawasiliano kati
ya binadamu na binadamu au jamii na jamii katika eneo fulani kama kabila au
taifa, na kadhalika. Hivyo basi, jukumu la kutimiza dhima ya kukidhi haja ya
mawasiliano katika jamii kupitia lugha haliwezi kutimia kama chombo hicho
(lugha) hakijaundiwa utaratibu maalumu. Utaratibu huo huundwa na wanajamii kwa
lengo la kuweka kaida au sheria zinazopaswa kuwaongoza watumiaji wa lugha hiyo
ili kuweza kufikisha ujumbe unaoeleweka. Utaratibu huo ndiyo unaoitwa sarufi ya lugha fulani.
Sarufi ni nini?
Kujibu
swali la sarufi ni nini, kunaweza kuchukua mamia ya miaka na rundo la maelezo
yaliyojazwa kwenye vitabu pamoja na vyanzo mbalimbali vya maarifa lakini bado
majibu yake yasifikie kikomo. Hii ni kwa sababu sarufi inahusu lugha; na lugha
yenyewe huendelea kupanuka kutoka vizazi hadi vizazi, na hivyo, kuifanya sarufi
nayo isiwe na kikomo cha kuifafanua. Maelezo haya yanaelekeza wazi kuwa sarufi
ni taaluma pana yenye mambo si haba kuhusu lugha. Kwa maana hiyo, kitabu hiki
hakiwezi kueleza kila kitu kuhusu sarufi bali kinagusia baadhi ya vipengele vya
sarufi ya Kiswahili ambavyo hupendekezwa kufundishwa katika elimu ya upili wa
chini hasa kwa shule za Tanzania. Mara baada ya maelezo haya mafupi ya
utangulizi ni muda mwafaka wa kujaribu kutazama majibu ya swali hili. Baadhi ya
wataalamu wa isimu (sarufi) wamejaribu kujibu nini maana ya sarufi kama
ifuatavyo:
Taasisi
ya Ukuzaji Mitaala (1988:28), wanaeleza sarufi kuwa ni mfumo wa taratibu na
kanuni zinazotawala matamshi, maumbo, miundo na maana katika lugha. Wanaendelea
kufafanua kuwa taratibu na kanuni hizi humwezesha mzawa au mtumiaji yeyote wa
lugha: 1) kutoa tungo sahihi na zinazoeleweka, 2) kuelewa tungo zinazotolewa na
mtu mwingine anayetumia lugha hiyo.Katika Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK, 2015:
912), sarufi imeelezwa kuwa ni tawi la isimu ya lugha linalojishughulisha na
fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia. Kwa ufupi, maana ya isimu katika
lugha ni taaluma inayochunguza na kuchambua mfumo na muundo wa lugha za
binadamu. Fonolojia ni sarufi matamshi inayohusika na uchunguzi pamoja na
uchambuzi wa utamkaji sauti za binadamukatika lugha husika; na, jinsi sauti
hizo zinavyotamkwa na mahali zinapotamkwa sambamba na vipashio vyake. Mofolojia
ni sarufi maumbo inayojihusisha na maumbo ya maneno katika lugha. Sintaksia ni
sarufi miundo inayochunguza miundo na mpangilio wa maneno katika lugha; nayo,
semantiki ni sarufi maana ambayo huchunguza maana katika lugha za binadamu.
Sambamba na maelezo ya Taasisi ya Ukuzaji Mitaala na Kamusi Kuu ya Kiswahili,Brinton(2000:8),
naye anasema kuwa “sarufi katika taaluma ya lugha, hutumika kurejea kanuni au
miongozo, ambayo hutawala lugha.” Kwa maana hiyo, na kwa mtazamo huu, sarufi ni
kanuni, sheria au taratibu ambazo lugha husika hujipambanua. Kanuni hizo ndizo
huongoza matumizi ya lugha. Kwa jumla, sarufi inaweza kufasiliwa kuwa ni kanuni
au taratibu zinazotawala na kuongoza matumizi ya lugha husika. Kanuni hizo
huwaongoza watumiaji wa lugha hiyo katika kutumia lugha kwa usahihi ikiwa ni
pamoja na kutunga na kuunda tungo sahihi na zinazokubalika katika mfumo wa
lugha ya jamii fulani.
Sarufi ya Kiswahili ni nini?
Kama
lilivyojibiwa swali la sarufi ni nini,
vivyo hivyo, ndivyo hata swali la Sarufi
ya Kiswahili ni nini linavyojibiwa, ikimaanishwa kuwa majibu yake
yanatokana na msingi wa kurejea wataalamu waliojishughulisha na sarufi ya
Kiswahili. Kama ilivyorejelewa mwanzo katika kujibu swali la maana ya sarufi,
vilevile Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (1988:28) wanasema kuwa Sarufi ya Kiswahili
ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matumizi sahihi ya matamshi ya
maneno, maumbo ya maneno, miundo ya tungo na maana ya miundo ya Kiswahili. Ni
mfumo wa taratibu zinazomwezesha mzungumzaji wa lugha ya Kiswahili kutoa tungo
sahihi za Kiswahili na pia zinazomwezesha mtu yeyote anayezungumza Kiswahili
kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetumia lugha ya Kiswahili.
Waaidha, Masebo na Nyangwine (2010:72) wanasema kwamba Sarufi ya Kiswahili ni
kanuni zinazotawala maumbo, matamshi, miundo na maana katika lugha ya
Kiswahili. Hivyo, sarufi ya Kiswahili, ni sarufi ambayo hujikita katika lugha
ya Kiswahili. Ni taratibu na miongozo ya utumiaji wa lugha ya Kiswahili.
Kutokana
na fasili ya sarufi ya Kiswahili, ni wazi kabisa kuwa sarufi ya lugha ya
Kiswahili huwasaidia wazungumzaji wa lugha hii kutambua miundo sahihi ya
sentensi wanazozitunga na maneno wanayoyaunda; kuelewa tungo zinazotungwa na
watumiaji wengine wa lugha ya Kiswahili. Sarufi ya Kiswahili imegawanyika
katika viwango (tanzu) vikuu vinne ambavyo ni: sarufi matamshi, sarufi maumbo, sarufi miundo na sarufi maana.
Viwango vya Sarufi ya Kiswahili
Neno
‘viwango’ hapa limetumika badala ya tanzu au matawi, au vipengele. Kwa hiyo,
viwango vya sarufi ya Kiswahili ni vipengele au tanzu au matawi ambayo sarufi
ya Kiswahili imegawanyika. Kama ilivyodokezwa, viwango hivi vipo vinne ambavyo
ni:
Sarufi Matamshi
Kwa
mujibu wa Kadeghe (2012:80), sarufi matamshi huchambua vitamkwa (fonimu) vya
lugha inayohusika, ikionesha namna na mahali kila kitamkwa kinapotamkwa. Neno
‘vitamkwa’ (kikiwa kimoja ni ‘kitamkwa[1]’) limetumika badala au
kumaanisha sauti zinazotamkwa katika lugha fulani.Naye Matinde (2012:58),
anasema sarufi matamshi ina wajibu wa kuchunguza na kufafanua sauti za lugha na
uamilifu wake katika mfumo mahususi. Anachokisema Matinde hapa, ni kwamba kazi
kubwa ya sarufi matamshi ni kuchunguza na kutoa ufafanuzi kuhusu utendaji kazi
wa sauti za binadamu katika lugha maalumu. Hivyo basi, sarufi matamshi ni
kiwango au kipengele cha sarufi kinachohusika na uchunguzi pamoja na uchambuzi
wa sauti za lugha mahususi. Sauti za lugha mahususi ina maana ya kuwa ni sauti
za lugha fulani kama Kiswahili, Kingoni, Kisukuma, Kinyarwanda, Kichina n.k.
Zinakuwa sauti maalumu au mahususi pale zinapobainishwa kuwa ni sauti za lugha
fulani kama mifano iliyotajwa hapa. Sarufi matamshi ya Kiswahili huchunguza
sauti za binadamu na utendaji kazi wake katika lugha ya Kiswahili – yaani,
huchunguza uamilifu wa sauti za lugha ya Kiswahili. Aidha, inachunguza na
kubainisha sifa za sauti, uamilifu wake na jinsi sauti hizo zinavyotamkwa na
kuambatana katika kuunda vipashio vikubwa zaidi ya fonimu; huchunguza namna na
mahali sauti hutamkiwa. Pia, Sarufi matamshi hujulikana kama fonolojia au
umbo-sauti.[2]
Sarufi Maumbo
Kamusi
Sanifu ya Isimu na Lugha (KSIL, 1990:40) inatoa fasili ya sarufi maumbo kuwa ni
“tawi la isimu (maana ya isimu
imefafanuliwa, rejea maana ya sarufi) ambalo huchunguza maneno na aina za
maneno.” Hiki ni kiwango au kipengelecha sarufi ambacho hujikita katika
uchunguzi wa maumbo ya maneno kwa kuzingatia uchunguzi wa miundo (jinsi
manenoyanavyoundwa) ya maneno, makundi ya maneno na uhusiano wa maneno pamoja
na taratibu za uundaji wa maneno. Sarufi maumbo ya Kiswahili huchunguza na
kuchambua maumbo ya maneno ya Kiswahili, na namna maumbo hayo yanavyotumika
kuunda maneno katika lugha ya Kiswahili pamoja na maana au dhana
zinazowakilishwa na maumbo hayo. Tawi hili la sarufi, hushughulikia uchunguzi
na uainishaji wa vipashio vya kimaumbo kama mofu na alomofu zake, viambishi,
mzizi, shina pamoja na uamilifu wa vipashio hivyo sambamba na mofimu za
vipashio hivyo (maana zinazobebwa na vipashio vilivyotajwa). Huchunguza pia
uainishaji wa aina za maneno kwa kuzingatia kigezo cha kimaumbo, kimuundo na
kimaana.
Sarufi Miundo
Hiki
ni kiwango cha sarufi kinachojulikana pia kama sintaksia. Massamba na wenzie
(2012:1) wanaeleza kuwa sarufi miundo ni utanzu wa sarufi unaojishughulisha na
uchanganuzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio
vyake. Nao TUKI (1990) wanafasili sarufi miundo kuwa ni tawi la isimu (sarufi)
linaloshughulikia uchanganuzi wa mpangilio na uhusiano wa vipashio katika kila
sentensi. Fasili za wataalam hawa zikichunguzwa kwa umakini zinabainisha kitu
kimoja au kilekile. Hii ni wazi kuwa sarufi miundo ni sarufi inayoshughulikia
miundo ya tungo katika lugha. Huchunguza mpangilio wa tungo katika lugha ya
binadamu na jinsi mpangilio huo unavyoweza kudokeza maana au dhana iliyolengwa
na iliyo sahihi.Sarufi miundo ya Kiswahili hujikita kwenye kuchunguza na
kuchambua miundo ya tungo za Kiswahili. Kwa maana hiyo, sarufi miundo si kitu
kingine bali ni kipengele cha sarufi chenye kujikita katika uchunguzi,
uchambuzi na ufafanuzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa
vipashio vyake. Fauka ya hayo, katika tawi hili la sarufi kinachochunguzwa ni
zile sheria au kanuni ambazo ni lazima zifuatwe katika kupanga maneno ya lugha
katika mfuatano kwa namna ambayo inafanya maneno hayo kuleta maana
inayokubalika na kueleweka katika lugha fulani. Huchunguza tungo kama neno
inavyoweza kuungana na tungo neno kuunda tungo kirai au tungo kishazi hadi
sentensi sanjari na kuchunguza viambajengo vinavyounda tungo hizi.
Sarufi Maana (Semantiki)
Sarufi
maana ya Kiswahili, kwa jina lingine hujulikana kama semantiki au umbo-sauti.[3] Wanaisimu Habwe na Karanja
(2004:201) wanafafanua sarufi maana kuwa ni utanzu wa sarufi unaochunguza maana
katika lugha ya mwanadamu. Vilevile, Mekacha (2011:13) anaeleza kuwa semantiki
ni taaluma inayochanganua na kufafanua miundo na mifumo ya maana na kipashio
chake cha msingi katika uchanganuzi ni leksimu, umbo lenye maana moja. Kwa
maana hiyo basi, ni dhahiri kuwa sarufi maana ni kipengele cha sarufi
kinachochunguza na kuchambua maana katika lugha za binadamu. Sarufi maana ya
Kiswahili huchunguza na kuchambua maana zinazokuwa zimebebwa na tungo katika
lugha ya Kiswahili. Maana zinazochunguzwa kwenye kiwango hiki cha sarufi ni
zile maana za maneno, vifungu vya maneno (kirai na kishazi) na sentensi. Hapa
ndipo wanasarufi (isimu) huchunguza na kuchambua nadharia mbalimbali
zinazofasili maana, aina za maana, jinsi ufasili wa watumiaji wa lugha huathiri
maana katika lugha. Kiwango hiki kimekua na kutanuka zaidi hadi kufikia hatua
ya kuzaa kipengele kingine kinachoitwa pragmatiki. Pragmatiki ni isimu
inayochunguza maana za usemi katika muktadha maalumu. Huchunguza jinsi maana
zinavyofasiliwa na wazungumzaji kulingana na mazingira ambamo mazungumzo hayo
hutokea. Japo kumekuwepo na mtazamo kwa baadhi ya wanaisimu kuipa hadhi ya
upekee kama utanzu wa isimu unaojitosheleza lakini mama mzazi wa pragmatiki
kama taaluma ya maana ni isimu maana (sarufi maana).
Hadi
kufika hapa, kwa kiasi fulani sarufi imeelezwa japo si kwa kirefu ila ufafanuzi
huu unatosha kutoa mwanga na uelewa wa dhana ya sarufi na vipengele vyake kwa
jumla.
Maswali
(a) Eleza
maana ya sarufi.
(b) Fafanua
kwa mifano sarufi ya Kiswahili maana yake ni nini?.
(c)
Taja
na ueleze kwa ufupi tanzu tano za sarufi ya Kiswahili
MAREJEO
BAKITA,Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK), Dar es
Salaam: Longhorn Publishers Limited,
2015.
Brinton, Laurel J, The Structure of Modern English: A linguistic Introduction,
Amsterdam:
John Benjamin Publishing
Company, 2000.
Habwe,
John na Peter Karanja, Misingi ya Sarufi
ya Kiswahili, Kenya: Phoenix Publishers,
2004.
Kadeghe,
Michael, Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Tanzania Kidato cha Kwanza,
Toleo la 3,Dar es Salaam:
Jamana Printers Limited, 2012.
Kihore,
Y. M., D. P. B. Massamba na Y. P. Msanjila, Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu
(SAMAKISA) Sekondari na Vyuo, Chapa ya 6, Dar es
Salaam: TUKI, 2012.
Mhilu, Greyson na Masebo J. A, Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha
Tatu, Dar es
Salaam:
Nyambari Nyangwine Publishers, 2010.
Matinde, Riro S, Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia, Mwanza: Serengeti Educational
Publishers (T) Ltd, 2013.
Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Kiswahili Sekondari, Dar es Salaam:
Kitabu Commercial Ltd,
1988.
TUKI,Kamusi
Sanifu ya Isimu na Lugha.Dar es Salaam: Eductational Publishers and
Distributors Ltd, 1990
[1]Kamusi Kuu ya Kiswahili inatoa fasili ya neno ‘kitamkwa’
kuwa ni kipande sauti katika mfumo wa lugha chenye sifa bainifu kis.:
fonimu.
[2]Rejea Y.M.Kihore na wenzake (2012:2)
[3]Wataalamu wa Isimu,Massamba na wenzie
(2012:30) na Kihore na wenzie (2012: 3) wanatumia istilahi ‘umbo-maana’
kurejelea dhana ya sarufi maana (semantiki).
0 maoni: