FASIHI
ASILI YA FASIHI SIMULIZI
Na
Alcheraus Mushumbwa
SAUT-MWANZA, Tanzania
2013
Maana ya Fasihi
Nakungah (2011 katika mtandao) anasema fasihi ni sanaa ya lugha iwasilishayo tajiriba zinazomwathiri binadamu. Misingi ya fasihi huwa katika ubunifu wa kuteua, kupanga na kunakili tajiriba mbalimbali za maisha. Kwake yeye, fasihi huhusika na udhihirishaji wa tajiriba za binadamu katika maisha yake.
Naye, Wanjala (2011:9), anafasili fasihi kuwa ni sanaa inayotumia lugha na matendo kuwasilisha ujumbe juu ya maisha ya binadamu. Huku, Bukagile na Ngambeki (2005:25), wanasema kwamba fasihi ni sanaa itumiayo lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii fulani.
Kwa upande wake Malenya (2012:40), fasihi ni sanaa maalumu ya matumizi ya lugha inayotoa mafunzo ambayo yanatumiwa kuieleza jamii. Msanii hutumia sanaa katika kuwasilisha ujumbe na kuhakikisha umewafikia wanaolengwa kupitia tanzu mbalimbali za kifasihi mathalani, hadithi, mafumbo, ngano, methali, mashairi, nyimbo na kadhalika.
Kwa fasili hizi za wanazuoni, ni kwamba, tunagundua kuwa wote katika fasili zao wanasisitiza mambo mawili muhimu: yaani, sanaa (ufundi) kama sifa au kitambulisho cha fasihi. Pia jambo lingine ni suala la lugha; ni lazima sanaa ya fasihi kwa upekee wake iendane na lugha ili kuweza kufikia lengo inalolinuia. Lakini sanaa hiyo hubeba ujumbe (maudhui) ambayo ndio msingi mkubwa wa kutoa sanaa hiyo, ujumbe huo hufikishwa kwa njia ya lugha. Lugha ni nguzo muhimu inayoitofautisha fasihi na sanaa nyinginezo.
Kwa hiyo tunaweza kuifasili fasihi kuwa ni sanaa au ujuzi (ufundi) unaodhihirika kupitia lugha na matendo ya binadamu hasa pale inapofikisha maudhui yake kwa walengwa (hadhira). Fasihi ni sanaa ambayo huwasilishwa kwa njia kuu mbili amabzo ni maandishi na masimulizi. Na hapa ndipo tunabaini aina za fasihi: yaani, fasihi simulizi na fasihi andishi. Fasihi simulizi ndio msingi mkuu wa fasihi. Hivyo basi tuangalie kwa undani fasihi simulizi.
Fasihi simulizi, ni fasihi ambayo hutolewa kwa njia ya maneno ya kuzungumza sambamba na matendo. Ni sanaa ambayo nyenzo kuu ya utunzi, uwasilishaji wake na usambazaji wake ni sauti pamoja na vitendo (Wanjala, 2011:13). Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake (Matteru, 2003:26). Fasihi ina asili yake, ambapo hapo ndipo tunang’amua chanzo chake. Zipo nadharia mbalimbali ambazo zimejaribu kuibuliwa na wataalamu zikieleza asili ya fasihi. Wanjala (2011) akimnukuu Mulokozi (1996) anasema kuwa tunaposema asili ya fasihi, inayozungumziwa ni fasihi simulizi kwani ndio mama mzazi wa fasihi andishi. Wanjala amebainisha nadharia nne zinazoeleza asili ya fasihi simulizi. Nitazieleza nadharia hizi kwa ufupi, kwa kuonesha dosari zake; halafu, nitatoa mtazamo wangu juu ya maelezo kuhusu nadharia hizo na mwisho kuhitimisha kwa msimamo wangu juu ya asili ya Fasihi Simulizi.
Kama ilivyodokezwa awali, tunaposema asili ya fasihi, tunaongelea fasihi simulizi; kama asemavyo Mulokozi kwenye andiko la “utafiti wa fasihi simulizi” kuwa, “uchunguzi katika fasihi simulizi unatuonyesha kuwa karibu tanzu zote za fasihi andishi tunazozifahamu na kujivunia leo zimechipuka kutokana na fasihi simulizi: karibu kila fani ya fasihi andishi ina ushabaha wake katika fasihi simulizi” (Mlokozi, katika Makala za semina ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili, 2003:19). Zifuatazo ni nadharia zinazodokeza asili ya fasihi simulizi kama alivyozibainisha Wanjala:
Nadharia ya udhanifu
Nadharia hii inaeleza kuwa asili ya fasihi ni Mungu. Inasadikika kuwa waasisi wake ni wasomi wa kale wa kiyunani, akiwemo Hesiod na Plato. Wanadai kuwa Mungu ndiye aliyempa binadamu msukumo wa kutunga kazi za kisanii, huyu Mungu ndiye mwenye kumwezesha msanii au kumpa uwezo wa kutunga kazi yake ya kisanii ikiwemo fasihi simulizi. Kwao, Mungu ndiye msanii mkuuu; kwani, usanii wake unajidhirisha katika ulimwengu alioumba. Na mwanadamu ni zao lake. Hivyo, kipaji cha kubuni sanaa kwa mwanadamu kimetoka kwa Mungu.
Dosari za nadharia hii kwa mujibu wa Wanjala (2011:10) ni kwamba inachanganya vitu viwili, yaani imani na taaluma na ni nadharia isiyo na uthibitishao wa kisayansi. Na hivyo, ni vigumu kuijadili kitaalamu. Vilevile inapuuza ukweli kwamba mazingira na jitihada za binadamu huwa na athari kubwa kwa binadamu katika kujitambua kupitia utamaduni wake.
Dosari hizi ziko wazi kabisa na pasipo uchunguzi wa kina waweza kuziacha kama zilivyo kwa kudhani kuwa zipo sahihi au si sahihi. Kwa mtu mwenye kupuuza uwepo wa Mungu, hakika ni sahihi kwake kwa kuziweka dosari hizi katika nadharia hii. Ila ni jambo la kutia dukuduku kama mtu anaamini uwepo wa Mungu na kukubali kuwa ndiye muumba wa kila kitu, halafu, anapuuza nadharia hii. Aidha, ni vigumu kujua moja kwa moja kama imani si sayansi, wakati imani ni njia moja wapo ya kupata maarifa. Na ni vigumu kukubali kuwa nadharia hii, haijadiliki kitaalamu, kwani wapo wanataaluma wa fasihi ambao ni waamini wakubwa wa Mungu na wanaamini uumbaji wa Mungu katika maisha ya binadamu. Wakati huo huo, tunajiuliza kuwa kama kila kitu kimeumbwa na Mungu, akiwemo binadamu, je huo uwezo na utambuzi alio nao mtu, unaotokana na mazingira na utamaduni wake uliomzunguka umetoka wapi kama si kwa Mungu aliyemuumba? Kwa ufupi kila nadharia haiwezi kujitoshereza kwa asilimia mia japo ukweli mkubwa unakuwemo.
Nadharia ya sihiri
Nadharia hii inaeleza kuwa sanaa imetokana na sihiri. Sihiri ni uwezo wa juu au nguvu za kimiujiza zaidi ya alizo nazo binadamu, ambazo hutumiwa na watu kufanya mambo yasiyo ya kawaida kwa uwezo wa kibinadamu. Waasisi wake wana muono kuwa sihiri imechukua nafasi ya sayansi katika ulimwengu wa sasa, hasa zama za kale, sihiri ilitumiwa na wanadamu katika kufanya mambo. Kwa hiyo fasihi na sanaa ni mazao yaliyochipuka kutokana na sihiri katika kujaribu kuyashinda mazingira. Kwa mfano ati, wawindaji wa zamani walichora kwanza picha ya mnyama amechomwa mishale, waliyetaka kumwinda kabla ya kwenda mwituni kuwinda wakiamini kuwa kitendo hicho kitatokea kweli, watakapofika msituni huku wakiimba. Na nyimbo walizoziimba katika kushadadia kitendo hicho ndio ushairi wa mwanzo.
Nadharia hii ina dosari kama ifuatavyo: kwamba yenyewe inachanganya dhima na asili ya fasihi. Kuwa, kutumika kwa ushairi katika sihiri hakumaanishi au hakudhibitishi kuwa sihiri ni chanzo cha fasihi. Nyimbo zilizotumika katika sihiri zilikuwa zinakamilisha azma yake kama inavyojitokeza katika shughuli mbalimbali. Mathalani, wasukuma huwa na nyimbo mbalimbali ambazo huwa nyenzo muhimu katika kufanya kazi, mfano kulima. Na hii haimaanishi kuwa nyimbo ndio kulima kwenyewe.
Nadharia ya wigo au uigaji
Nadharia hii husisitiza kwamba binadamu ni mwigaji wa maumbile ya maisha yanayomzunguka. Plato, naye Aristotle, ni waasisi wa nadharia hii. Plato akisisitiza kwamba wasanii wa sanaa huiga mambo halisi ya ulimwengu halisi, ambao wengi waliyatafsiri kama mazingira ya mbinguni. Na hivyo, wasanii hao wanaupotosha ukweli wa mabo halisi yalivyo. Wataalamu wengine wa fasihi, wameiita nadharia hii kuwa ni nadharia ya umithilishaji. Kwa mtazamo huu, fasihi hufafanuliwa kuwa chanzo chake ni umithilishaji katika uhusiano wake na maisha; kwa kuiona kama njia ya kujenga au kuhusisha tukio au hali fulani ya maisha kwa kutumia mchoro na rangi. (Nakungah, tar. 12, Juni, 2011, mtandaoni) akimsimulia Aristotle, huku akimnukuu Abrams (1981), anasema kuwa “katika kazi yake ya `Poetics', Aristotle anaeleza ushairi kama umithilishaji wa vitendo vya mwanadamu. Kwa `umithilishaji' anamaanisha `uwakilishi', kwa misingi yake. Kwa hivyo, kwa maoni ya Aristotle, shairi humithilisha kwa kuchukua kitendo fulani cha mwanadamu na kukionyesha upya katika `mtambo' mpya - ule wa maneno”. Kwa mantiki hii, ni kwamba fasihi huweza kuiga na kumithilisha maisha.
Moja wapo ya dosari ya nadharia hii, ni kwamba, inasisitiza sana kuiga na kusahau suala la ubunifu, amabalo ndio uti wa mgongo katika sanaa na fasihi. Dosari hii yaonekana pakubwa kuwa na mashiko lakini, nadharia ya umithilishaji au wigo ikitafakariwa kwa kina, itagundulika kuwa ni wazi kabisa kwamba japo tunasema mwanadamu anao uwezo wa kubuni; ni kweli, lakini yafaa tujiulize kama kubuni huko si zao la wigo, msanii huyo anaiga kutoka wapi wakati akiishi katika mazingira? Binadamu anaiga mazingira yake aliyoyakuta, kama ahigi basi yeye ndiye atakuwa muumbaji wa mazingira hayo; jambo ambalo si kweli. Kuiga si jambo amabalo mwanadamu analifanya kutoka katika ombwe tupu, bali anaiga kutokana na mazingira anamoishi na mazingira hayo hakuyaumba yeye. Katika kubuni huko, msanii humithilisha uhalisia wa mambo ambayo kwa uwezo wake hawezi kuyawakilisha kama yalivyo kwa uhalisia wake. Mfano kitendawili kama “nyumba yangu haina mlango, ‘yai’ ”. Kitendawili hiki kina umithili ndani yake. Kwamba kilicholengwa hapa ni ‘yai’, lakini linawakilishwa kwa picha ya nyumba isiyo na mlango. Hakika hakuna nyumba isiyo na mlango, ila kwa msanii kutaka kutumia sanaa analichukulia yai mithili ya nyumba; yaani kwa maneno mengine anaiga nyumba kuelezea yai, wala yai si nyumba ki uhalisia.
Nadharia ya kiyakinifu
Hii ni natharia ya mtazamo wa ki-marx; ambayo inayaangalia maisha kwa uyakinifu. Karl Marx na Engel ni waasisi wa nadharia hii (Wanjala 2011:11). Msisitizo wake ni juu ya chanzo cha binadamu, kuwa, ni zao la maumbile asili ya ulimwengu na akaanza kubadilika taratibu kulingana na mazingira. Mabadiliko hayo ni katika nyanja zote za maisha, mfano utamaduni, falsafa, lugha na fasihi. Katika mabadiliko hayo, mwanadamu alianza kugundua kuwa anaastahili kuratibu mazingira katika shughuli zake ili aweze kuthibiti mazingira vizuri. Na lugha ilianza kama njia ya kurahisisha uratibu huo kwa mawasiliano na baadae lugha ikawa chombo cha sanaa, ambayo ni fasihi. Na hapo fasihi ikaanza kujitenga na shughuli za uzalishaji, ikiwa ni sanaa ya burudani na shughuli maalumu za kijamii kwa mfano sherehe na ibada. Na huo ukawa mwanzo wa fasihi.
Dosari moja wapo ya nadharia hii, ni kuipa uwezo mkubwa lugha kuwa ndio sanaa, jambo ambalo kimantiki si sahihi. Bali, lugha ni njia moja wapo ya kuieleza sanaa ya fasihi na wala lugha tu haitoshi kuwa sanaa pekee. Sanaa ni picha ya ufundi ya kuwakilisha lengo fulani. Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa maandishi, michoro na uchoraji au uchongaji (Kamusi ya Kiswahili Sanifu). Kwa hiyo, lugha si sanaa kama wanavyosisitiza waasisi wa nadharia hii; bali, ni njia moja wapo ya kuieleza au kuitoa sanaa, ambapo fasihi kama sanaa yenyewe huwasilishwa kwa lugha.(dosari hii nimeibainisha mwenyewe).
Baada ya kuangalia mawazo ya wataalamu mbailimbali juu ya asili ya fasihi simulizi au fasihi kwa ujumla, hasa, kupitia nadharia zao; ni vema sasa, tuone mawazo ambayo yaweza kuwa mbadala wa nadharia hizi, yakilenga kuleta changamoto kwa nadharia hizi na kueleza asili na chanzo cha fasihi. Na hii ni baada ya kuzitafakari nadharia zilizoelezwa na kupata mkanganyiko. Na pengine mtazamo huu waweza kutupa mawazo mengine ambayo yaweza kuelekea katika ukweli wa asili ya fasihi.
Asili na Chanzo cha Fasihi ni Binadamu
Fasihi simulizi asili yake ni mwanadamu hasa alipoanza kuongea na kutumia lugha kueleza hisia na mawazo yake kwa wengine. Tunaposema asili ya fasihi ni binadamu, ina maana ya kuwa sanaa yoyote ile, fasihi ikiwa ni mojawapo, ni matokeo ya binadamu kudhihirisha uwezo wake alio nao katika kutumia akili yake kuyamudu maisha. Sanaa kwa ufupi ni ufundi; ufundi ni kipaji cha asili alichonacho msanii (binadamu), na kwa kuwa akili ndiyo imuongozayo mtu katika kutimiza jambo, basi hutumia kipaji hicho katika kuhakikisha anayaishi na kuyamudu vema maisha yake. Fasihi na sanaa nyingine ni matokeo ya mwanadamu kutumia vema akili yake katika kuishi na kuyamudu mazingira yake. Mwanadamu ndiye kiumbe mwenye akili zaidi hapa duniani. Na kwa kuwa ana akili, binadamu hutumia akili hiyo kuweza kufanya mambo mengi ikiwemo kuonesha utaalamu wake (sanaa) wa kipekee kwetu.
Fasihi na sanaa nyinginezo, ni matokeo ya binadamu mwenye uwezo wa kutumia akili yake katika kuishi. Sanaa kama uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, udarizi, muziki na kadhalika, ni mazao au matokeo ya akili ya binadamu, imtumayo kuchora, kufinyanga, kuchonga, kutengeneza ala za muziki nakadhalika. Hii inatokea pale yeye aonapo kuwa anahitaji kufikisha malengo yake kwa wanadamu wenzie, basi si budi kwake kutumia mbinu hizi kueleza mawazo yake kwa wengine. Hivyo hivyo, kwa fashi ijitengayo na sanaa hizi kwa nyenzo ya lugha. Lugha ni chombo kinachomhusu binadamu, ambapo sauti za zilizo katika mpangilio maalumu na zilizokubaliwa na jamii hutumika katika maisha ya kila siku kwa ajili ya mawasiliano. Hivyo baada ya kutumia sanaa nyingine ambazo ni kama ishara pekee kuwasilisha azma ya msanii, binadamu akaamua kuunda lugha na kuitumia kufikisha ujumbe wake. Na hilo ndilo chimbuko la fasihi. Kwa kuwa huyu binadamu ana akili, mwanzoni akitumia sanaa nyingine, akaamua pia kuibua ubinfu mwigine, ambapo akatumia masimulizi, yaani maneno katika kuumba na kuwasilisha sanaa yake; nayo ni fasihi simulizi. Kwa hiyo sanaa au fasihi, isichukuliwe kama kitu kilicho katika ombwe tupu au kitu kilichokuwepo kabla hata binadamu hajawepo, la hasha, fasihi na sanaa vimekuwepo baada ya binadamu na ni zao la binadamu mwenye kuyatawala maisha. Kwa hiyo, mawe, milima, bahari na mambo mengine ya asili si sanaa, bali ni asili. Sanaa ni matokeo ya binadamu kutumia asili hiyo.
Mawazo haya yaweza kukutana na upinzani wa hoja mbalimbali ikiwemo ya Mungu kumuumba mwanadamu na kumpatia uwezo wa kumiliki mazingira. Ni kweli Mungu alimuumba mwanadamu na kumpa akili na kumuacha atumie akili yake kuishi; na kama binadamu angepewa kila kitu, basi yeye asingelikuwa anaangaika na kumiliki mazingira yake. Mungu hakumpa binadamu kila kitu; kama ni hivyo, basi hata dhambi atendazo mtu kapewa kwa uwezo wa Mungu. Ila si kweli, Mungu alimpa mtu utashi na akili, kupitia vitu hivi viwili binadamu hupaswa kuvitumia na kuibua mambo mbalimbali. Na kwa hiyo, sanaa na fasihi ni matokeo ya matumizi ya akili na utashi. Kama binadamu asingeliamua na kuchagua kuwa mbunifu au kutumia lugha kwa mawasiliano; asingelifanya hivyo na leo hii tusingelikuwa tunasigana kuhusu fasihi.
Kwa kuhitimisha, ni kwamba, pasipo binadamu, hakuna sanaa, kwani hata nadharia zote zinazoeleza chanzo cha fasihi hazimtupi mwanadamu japo zinakwepa kumbainisha moja kwa moja. Chimerah na Njogu (1999:142), wanadhihirisha wazi kuwa fasihi ni ya binadamu hasa wasemapo kuwa, “kwa vile fasihi simulizi inapata kubuniwa kutokana na mazingira ya wanajamii (binadamu) na tabia zao hao wanajamii, basi tunakuta ya kwamba, tangu kuwepo kwa binadamu ulimwenguni, fasihi nayo imekuwepo na imeeleza mambo aina aina katika nyanja mbalimbali za taaluma, kama vile taaluma; kama vile lugha, fasihi andishi, historia, jiografia, falsafa (busara), maadili, elimu na hata sayansi.”
Kwa mantiki hii, hatuwezi kupata fasihi pekee pasi na binadamu. Na kwa maana hiyo, ndio maana fasihi simulizi ni sanaa inayobuniwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa lugha (ya mdomo). Vyombo vyake vikubwa ni mdomo na sauti ya binadamu katika hali ya kuimba, kusimulia, kuiga, kughani, kutamba, kutega na kadhalika – miradi yake yote yanatolewa kwa mdomo na ishara za mwili (Mazrui na Syambo, 1992:2). Kwa ufupi ni kuwa hakuna namna yoyote utaongelea fasihi simulizi au andishi, usimhusishe mwanadamu. Na hivyo, fasihi haipo pasipo binadamu. Fasihi simulizi ni zao la mwanadamu kuanza kuzungumza, na hasa kuamua kueleza sanaa au kazi zake kwa lugha; yaani, masimulizi.
Marejeo
Bukagile, G.R na Ngambeki, J (2005). Kiswahili kwa Shule za Sekondari. Dar es Salaam:
General Booksellers Ltd.
Mazrui, A.M na Syambo, B.K (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African
Educational Publishers.
Malenya, M.M (2012). Matumizi ya Lugha katika Fasihi Simulizi (nyimbo za Jcob
Luseno). Toleo la 1. Mwanza: Inland Press.
Njogu, K na Chimerah, R (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
Wanjala, S.F (2011). Kitovu cha Fasihi Simulizi, kwa shule, vyuo na nadaki. Mwanza:
Serengeti Bookshop.
TUKI (2003). Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III. Fasihi.
Toleo la 2.Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nakungah, Kiswahili Taalamifu “Fasihi Simulizi” tarehe 21, June 2011. http://kiswahilitaalamifunyangeri-nakungah.blogspot.com/2011/06/fasihi-simulizi.html (imetembelewa, 22. 2. 2014: saa 2:16 asubuhi).

0 maoni: