*Kiu ya Chuo*
Akiwa ameketi  katika mkeka mchafu  uliotandikwa chini ya   Mfenesi alijikuta akitililikwa na machozi mithili ya mtu aliye fiwa.Hata hivyo machozi hayakufifisha mvuto wa macho ya kimahaba ya Sikujua. Sikujua alikuwa binti mrembo wakuvutia,urefu na unene wake wa wasitani,miguu mizuri iliyounganishwa na mapaja manene ambayo yalishikilia barabara makalio makubwa vilimfanya arushe roho za marijali.Kiuno cha Sikujua kilijikata vema,tumbo dogo na chuchu za saa sita mchana zilipamba kifua cha kigori huyu.Shingo yake ilikamatilia sawasawa kichwa chenye nywele ndefu.Uso wa duara rangi ya Maji ya kunde ulionakishiwa na puwa ndefu ndefu,macho   na mdomo mdogo vilikamilisha umbile timamu la Sikujua.
"Bibie vipi watokwa na machozi?!"nilihoji huku nikimtazama kwa jicho lakipekuzi.
" Kaka yangu dunia si yangu tena,kila kitu kimesambaratika sina kesho yangu nimevurunda kila kitu kaka yangu" Sikujua alijibu huku akigugumia kwa kwikwi ya kilio.
"Bado umeniweka gizani dada yangu,nieleze kipi hasa kilichokusibu?" niliendelea kumsaili.
"Kiu ya Chuo imenitokea puani"
"Kivipi Dada?"
"Kaka niliamini mwisho mwema hutakatisha njia kumbe la ,njia sahihi ndio huleta mwisho mwema." Alijibu huku akijifuta machozi kwa kitambaa.
"Unazidi kuniweka njia panda Sikujua"nilidodosa.
Basi Sikujua anza kunisimulia."Mimi nimezaliwa katika familia duni,baba ni mkulima wa bustani ya nyanya na vitunguu.Mama ni fundi mfinyazi wa vyungu.Kipato cha nyumbani ni cha kulenga na manati,kula yetu yenyewe moja kwa kutwa.Nakumbuka enzi nasoma shule ya msingi mama alikuwa akinipikia viazi au mihogo na wakati mwingine Matoborwa jioni, na asubuhi aliniwekea katika mkoba wa shule.Ilikuwa ni utaratibu wa kila siku kubeba chakula cha kula mchana kwani hapa kuwa na fedha ya kunipa ili ninunue chakula niwapo shule.Nilisoma kwa tabu sana kaka yangu.Nguo za shule nilinunuliwa Mara moja kila baada ya miaka miwili.Mama alikuwa akinishonea kwasindano ya mkono na uzi wa sandarusi kuziba matobomatobo katika sare zangu za shule.Hali ya maisha ya wazazi wangu imekuwa ngumu kwa muda mrefu sana.Baba anapokosa fedha ya kununulia chakula huwa hana budi kutafuta kibarua chochote ili sisi familia yake mikono iende kinywani.Kilimo chake cha nyanya ni duni hana mtaji wakutosha,pembejeo ni duni na wala hakuna cha  bwana shamba wala bibi shamba hivyo baba anafanya Kilimo cha kienyeji sana.
Pamoja na milima na mabonde yote niliyokuwa na kutana nayo katika safari yangu ya kielimu nilijikaza hatimae nikafanikiwa kujiunga shule ya sekondari.Sitasahau Furaha niliyoipata siku ile napewa taarifa kuwa nimechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Tembo." Hongera sana Sikujua umefaulu na umechaguliwa kujiunga Tembo" ilikuwa ni sauti ya Mwalimu Sijaona.Moyo wangu ulilipuka kwa furaha hali iliyofanya mwili wangu kusisimuka kutokana na hisia tamu za burudiko lilomea nafsini mwangu.Taarifa za kufaulu kwangu kwa wazazi wangu zilileta furaha iliyochanganyikana na hofu.Hofu ya wazazi wangu ilikuwa ya kimsingi kabisa baba alijikuta njia panda; kunipeleka shule au kukacha.Ada ya shule na michango mingine pamoja na sare za shule ilikuwa mtihani mzito." Mwanangu umefaulu hongera,lakini tutafanyeje sasa ikiwa kula yenyewe inatushinda?!,samahani mwanangu",maneno ya baba yalinichoma mkuki moyoni kwani haya kuwa ya matumaini kabisa.Furaha yangu iligeuka huzuni ghafla.Lakini mama alimtia moyo baba." Baba Sikujua usiseme hivyo unamkatisha tamaa mwanao,kashatutoa kimasomaso wazazi wake.Ni wajibu wetu kuhakikisha anakwenda shule,huwezi jua huyu anaweza kuwa mkombozi wetu wa baadae.Hebu tazama tangu tukiwa vijana hadi sasa uzee unatunyemelea bado ufukara unatuadhibu! Kilichobaki sasa tufanye chochote kumwendeleza mwanetu kipenzi wapekee."Mama alirejesha tumaini langu.Baba alipumua kwa nguvu ahuuu!kisha akanishika bega la kushoto mwanangu nakupenda sana nitafanya lolote liwezekanalo kukusomesha hadi ufikie ndoto zako.Mama yako na mimi tu nakutegemea wewe.Wewe Sikujua kuanzia sasa ni tumaini letu.Sikujua..! aliniita huku akinitazama usoni.Labeka baba! Nilitika.Wewe ni Tumaini.Baba aliongea kwa msisitizo.Tangu hapo nilianza kusoma kwa bidii sana.Nilielewa wazazi wangu waliamini Mimi ndio n itakuwa msaada wao kwa baadae na ili niweze kuwa tumaini la kweli la wazazi wangu hapakuwa na budi kufaulu mtihani wa kidato cha nne.Nilijijengea nidhamu,niliwaheshimu walimu nao wakanipenda.Jembe halimtupi mkulima kaka hatimae nilifaulu na kujiunga kidato cha tano ambako nako nilifanikiwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita.Kiu yangu kuu ulikuwa ni kusoma Chuo kikuu,ndoto yangu ni kuwa dakitari lakini...lakini...ni..ni..nikama nimepoteza kila kitu! Sina thamani tena,nimewaangusha wazazi wangu.Mimi sio Tumaini."Sikujua alijikitu machozi na kilio kikuu vikimkaba koo akakosa la kuongea zaidi ya kumwaga kilio cha kusaga na meno.Nami niliamua kumwacha alie ili kutoa hisia za maumivu aliyokuwa nayo.Tayari niling'amua bila shaka kuwa Sikujua alikuwa amekabiliwa na masaibu makubwa.Kwa wakati ule ilifaa kumwacha alie kisha akinyamaza mazungumzo yaendelee.Taaluma ya ualimu niliyosomea hasa somo la ushauri nasaha lilinisaidia sana.Wakati Sikujua unaendelea kulia nikajiahidi kumsaidia kwani tiba ya tatizo lake ni usadi tu."Hapa ushauri nasaha unahitajika" nilijisemea moyoni.
Baada ya kitambo kidogo Sikujua alinyamaza kulia.Mazungumzo yetu yakaendelea."Sikujua nini kimetokea hata usiwe Tumaini tena?!"nilihoji."Kaka yangu nilipohitimu kidato cha sita hali ya kiuchumi nyumbani ikawa mbaya zaidi ya mwanzo baba anaumwa madonda ya tumbo hawezi tena kufanya kazi ngumu.Mama ndo anahudumia familia.Kipato cha mama ni kidogo hakiwezi hata kukidhi mahitaji muhimu nyumbani.Ufukara umevamia familia yetu.Baba anahitaji fedha ya matibabu mimi nahitaji fedha ya ada ya Chuo."Sasa si ungeomba mkopo wa serikali?"  nilimuuliza Sikujua huku nimemkodolea macho."Kaka yangu niliomba lakini sikufanikiwa,siku ya kufa nyani miti yote huteleza."Sikujua alisisitiza."Duh! Hii nchi nayo inamaajabu yake,ama kweli ukisitaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni;hivi inawezekanaje ukose mkopo ilihali watu wanaotoka familia bora wanapewa?!."nilijikuta nikimuuliza swali ambalo lilikuwa nje ya uwezo wake."Ndo hivyo kaka yangu.Baada ya kuona hivyo ikanibidi niende mjini kutafuta japo kijikazi cha kuniingizia kipato cha kujikimu.Mjini nako mambo hayakuniendea vizuri kwani nilitanga huku na kule bila kupata kazi ya maana hatimae nikaamua kufanya kazi baani! Yaani kaka yangu..." Sikujua alishindwa kumalizia badala yake alianzakulia tena.Awamu hii nilichukua kitambaa changu na kuaanza kumfuta machozi yaliyokuwa yakitiririka mashavuni pake mithili ya maji ya bomba.Kisha akaendelea;Kazi ya kuuza vinywaji inachangamoto zake.Kwanza unafanyakazi hadi usiku wa manane, ujira kidogo, kero za walevi na hatari ya vishawishi.Nilijitahidi kuvumilia yote ili tu niweze kupata chochote kitu nijikimu na kumusaidia mama kutunza familia nyumbani.Siku moja  nikiwa kazini alifika mteja mmoja aliejiita Sijali na kuomba nimuhudumie.Bwana sijali alikuwa ni mtu wa makamo apatae miaka arobaini hivi,ni mtu alieonekana kujiweza kifedha.Kwa nje alionekana mtu mpole, mcheshi na mwenye huruma lakini kumbe ni mkatili asie na mfano.Sijali ameniachia donda ndugu, ameyafanya maisha yangu yakose thamani yaani sikujua kama Sijali angenifanyia hivi.Upole na usikivu aliouonesha Sijali kwa nje ulinilaghai akili nikaamini angeweza kunisaidia.Nilimsimulia mkasa wa maisha yangu na ya familia pamoja na kiu yangu ya chuo.Sijali aliniahidi kunisaidia siku hiyo aliniachia namba ya simu akinisistiza nimtafute kesho yake ili anielekeze atakapokuwa ili tukutane na aone jinsi ya kunisaidia.Kesho yake ilipofika nilimtafuta na akanielekeza alipo nilienda lakini chakushangaza nilimkuta peke yake nyumbani nilipo muuliza alidai mkewe na watoto walikuwa wamesafiri.Alinikaribisha sharubati iliyo kuwa imejaa katika bilauri ndefu, nilishukuru kisha nikaanza kunywa.Kaka yangu sikujua kilichoendelea baada ya hapo badala yake ilikuwa ni kufumba na kufumbua nikajiona nipo chumbani kwake na bwana Sijali sote tukiwa uchi wa mnyama.Kitanda tayari kilikuwa kimesambaratika hali iliyo onesha dhahiri kuwa kazi aliyokusudia Sijali ilikuwa imekamilika.Si kuwa na la kufanya zaidi ya kulia kilio kisicho na msaada.Sijali alikuwa kimya akinitazama tu.Niliamua kuvaa nguo na kuondoka lakini kabla sijafika mbali aliniita; "Sikujua tafadhali simama". Nilisimama." Tafadhali shika zawadi yako".Sijali alinipatia bahasha ya kaki,wala Sikujua kulikuwa na zawadi gani ndani ya bahasha ile kwa wakati ule hadi nilipo fika nyumbani na kuifungua.Nilipofungua sikuamini macho yangu,kulikuwa na vipande viwili vya karatasi kimoja kilikuwa ni hundi ya milioni tatu na cha pili kilikuwa na ujumbe wa maneno uliochoma moyo wangu.Ujumbe ulisema: "Sikujua Mimi Sijali ndoto za mtu nacho jali Mimi ni adhima yangu ya kukidhi haja zangu.Hata hivyo nimekupenda nimeaamua nikusaidie hiyo fedha ukasome ili ukate kiu yako ya chuo.Napenda utambue wazi pia Mimi sio mzima kwahyo wewe pia kwa sasa si mzima.Mimi na wewe tuna Virusi vya Ukimwi. Wengi nimewaambukiza lakini Sijali, kwani nani ajuae kuathirika kwangu? Niliambukizwa na wanawake nami lazima niwaambukize.Pole Sikujua kwa kuwa miongoni mwa orodha yangu." ....Sikujua hakuendelea tena kusimulia kwani kwikwi na kilio kilimzidi.Nilimwacha hadi aliponyamaza mwenyewe ndipo nilipo anza kumtia moyo dada yangu huyu wa hiyari.Ukimwi sio mwisho wa maisha,ipo njia ya kuishi kwa matumaini.Kinachotakiwa nikupiga moyo konde maisha lazima yaendelee na ndoto sharti kuifikia.Zote ni changamoto za maisha kuzikabili hakuna budi.Mazungumzo yangu na Sikujua yalikuwa ni tiba kwake alitoa sumu zote akawa salama kihisia. Tangu siku hiyo hadi sasa Sikujua ni mtu mwenye furaha maishani.Mwaka uliofuata alipata ufadhili wa masomo toka shirika fulani la kidini akaenda kusoma udaktari chuo kimoja nchini Ujerumani.Aliporejea kaanza kufanya kazi yake vizuri.

Mtunzi: Manyuka, M.K
Mawasiliano: 0764419640/ manyukakapaya@gmail.com
DHNA YA SENTENSI: MTAZAMO WA KIISIMU

Sentensi
Sentensi ni kipashio kikubwa kabisa cha kimuundo chenye maana kamili. (Massamba na wenzake, 2012:136). Nao Roberts N. B na Spancer A (2007:3) wanaeleza kwa kimombo kuwa “sentensi ni mpangilio au mfuatano wa maneno ambao huanza na herufi kubwa na kuishia kwa kituo kikubwa, ambapo kwa kawaida hutumika kuelezea au kufafanua hali ya mambo au vitu duniani.” (Tafsiri ni yangu)
Fasili hizi ni sahihi kabisa na kwa mwelekeo huo, tunaongezea kwa kusema kuwa sentensi ni kiwango cha juu kabisha katika viwango-madarajia ya tungo; ambacho, kwacho kinakuwa na maana iliyotimilika.
Sifa za sentensi
Sentensi zinazo sifa zake ambazo zinazisheheni ndani kwa ndani kama zikichunguzwa kwa undani kwa jicho la kisarufi zaidi. Baadhi ya sifa hizo, ni hizi zilizoorodheshwa:
i. Sentensi ni tungo ya kiwango cha juu kabisa katika viwango vya tungo.
ii. Sentensi zinajibainisha zaidi kimuundo. Hii ina maana ya kuwa sentensi hujistili na kupata uamilifu wake hasa ikitazamwa au kuchunguzwa katika sarufi miundo (sintaksia).
iii. Sentensi ni kipashio chenye maana iliyokamilika.
iv. Sentensi zina miundo yake mbalimbali.
v. Sentensi za Kiswahili zina miundo yake mahususi (taz. SAMIKISA, 2012:137-152).
vi. Sentensi ni utungo ambayo una sehemu kuu mbili, yaani mtenda na mtendwa (kiima na kiarifu au kikundi nomino na kikundi kitenzi/ kirai nomino na kirai kitenzi).
Hizi ni baadhi ya sifa bainifu za tungo sentensi ambazo kwa kiasi kila sentensi huwa nazo.
Aina za sentensi
Sentensi kama tungo, zinajibainisha kwa aina zake. Na aina hizi za sentensi zineainishwa katika mitazamo miwili tofauti ambayo ni mtazamo wa uainishaji sentensi kimuundo na mtazamo wa uainishaji sentensi kimaana.
Uainisha wa sentensi kimuundo
Uainishaji huure wa tungo sentensi huzingatia muundo (au umbo ) wa sentensi zaidi. Katika uainishaji huu tunapata aina nne (4) za sentensi, ambazo ni:
Sentensi sahili;
Sentensi ambatani;
Sentensi changamani.
Sentensi shurutia.
Kwa uanishaji wa kimuundo, sentensi zilizotajwa hapo juu ndizo aina za sentensi. Ikumbukwe kuwa hapa sentensi zimeainishwa kimuundo na si vinginevyo.
1. Sentensi sahili/huru
Habwe na Karanja wanasema kuwa hii ni sentensi ambayo ina kitenzi kikuu kimoja. Wakiwa na msisitizo kwamba sentensi ya/za aina hii si lazima zi/iwe rahisi kueleweka kimaana au zi/iwe fupi katika muundo wake. Ni sentensi yenye kueleza wazo moja tu ambalo hubebwa na kishazi kikuu hicho. Na Massamba na wenzie, wanafasili aina hii ya sentensi kwamba ni muundo wa tungo-sentensi unaohusisha kirai-nomino na kirai-kitenzi, na wenye maana kamili iliyokusudiwa. Kwa hiyo, sentensi sahili ni sentensi ambayo ina muundo wa kikundi-nomino na kikundi-tenzi yenye maana kamili iliyobebwa ndani ya wazo moja lililokusudiwa.
Mifano:
a) Baba ananipenda sana.
b) Kuku wangu ametotoa vifaranga vingi.
c) Anatembea.
d) Huyu ni mwalimu.
e) Marwa anasoma sana.n.k.
Mifano iliyobainishwa hapo juu ni sentensi sahili/sentensi huru, ambazo zina kikundi-nomino na kikundi-kitenzi na pia zimebeba maana na wazo moja lililokusudiwa. Sentensi sahili zina miundo yake. Na hii ifuatayo ni miundo ya sentensi sahili:
a) Muundo wa kirai-kitenzi.
- Nimekula.
- Anacheza.
- Wanalima.
Katika muundo huu, kirai-kitenzi kimesimama pekee kama sentensi sahili na kirai-kitenzi kimeundwa na kitenzi kimoja tu.
b) Muundo wa kirai- nomino na kirai-kitenzi.
- Felista anakuja.
- Vijana wanasoma.
- Wanakwaya wanaimba.
Kwenye sentensi hizi, inabainika wazi ya kwamba sentensi hizi zimeundwa na kirai-nomino kimoja na kirai-kitenzi kimoja.
c) Muundo wa virai-nomino na virai vitenzi vilivyokitwa katika kitenzi ‘kuwa’.
- Abasi ni kijana mzuri.
- Rugaenda yumo dukani.
- Abedi alikuwa kijana mwadilifu.
- Mwalimu atakuwa darasani kesho.
- Jane alikuwa na pesa.
- Kaka angekuwa wa kwanza.
Katika mifano ya sentensi iliyotolewa hapo juu, vitenzi vyake huchukuliwa kama miundo ya kitenzi kuwa katika wakati uliopo, na miundo hii yote inapowekwa katika nyakati tofauti nafasi yake huchukuliwa na kitenzi kuwa.
d) Muundo wa virai-nomino na virai-vitenzi vilivyoandamana na vijalizo.
- Dada yangu alinunua mayai matata usubuhi.
- Liliani anatafuta nguo yake kabatini.
- Mrembo mzuri alinyeshewa mvua nyingi jioni.
Katika muundo huu virai-nomino vina nomino na vivumishi mbalimbali na virai-vitenzi vimefuatwa na vijalizo ambavyo ni nomino, vielezi na vivumishi.
2. Sentensi ambatani
Sentensi ambatani ni tungo iliyo na tungo mbili zilizounganishwa na kiunganishi. Ni sentensi moja iliyounganishawa na vishazi huru viwili. (Taz. Misingi ya Sarufi na SAMIKISA).Aina hii ya sentensi hubeba visha viwili ambavyo huwa vinaendana kimaana.
Mifano:
a. Wanachuo wa Katoke ni wasikivu ilhali wanachuo wa Butimba ni wakorofi.
b. Anita anawabishia walimu lakini Roda anawasilikiza.
c. Mwalimu Mustafa ni rafiki wa mwalimu Lackson na mwalimu James ni rafiki wa mwalimu Jonia.
d. Wanachuo wa mwaka wa kwanza wanafagia viwanja huku wanachuo wa mwaka wa pili wanafyeka.
Ukichinguza mifano hii, utaona kuwa kila tungo inajumuisha sentensi mbili ambazo ni huru na zikiunganishwa na kiunganishai kimoja. Viunganishi katika sentensi hizi ni ilhali, na, lakini na huku. Sasa tuone mifano ya miundo ya sentensi ambatani:
a) Muundo wa vishazi sahili tu (sentensi sahili zilizounganishwa).
- Amepigwa sana lakini hajaumia kupita kiasi
- Tutangulie na wao watufuate.
- Siogopi wala sitishiki.
Hapa sentensi zilizotungwa ni sentensi ambatani ambazo kila sentensi imeundwa na sentensi sahili mbili zilizounganishwa na kiunganishi.
b) Muundo wa vishazi sahili na changamani (sentensi sahili na changamani).
- Wazazi waliokuwa hapa asubuhi wamerudi kwao lakini watoto wao hawakurudi.
- Chakula kizuri kimeiva wakati mpishi aliyekipika ameondoka.
- Wanafunzi wangu wameshindwa kufaulu mtihani lakini wale waliokuwa wamerudishwa kwao wamefaulu vizuri.
Katika sentensi hizi ni wazi kuwa sentensi sahili zimeambatana na sentensi changamani. Sentensi sahili ni vishazi huru na sentensi changamani ni vishazi changamani. Vishazi changamani vinadhihirishwa na urejeshi.
c) Muundo wa vishazi changamani tu (sentensi changamani zilizoungana)
- Ng’ombe aliyevimbiwa baada ya kula nyasi nyingi amechinjwa lakini mbuzi waliovimbiwa wamekufa.
- Vijana wale waliokuja hapa asubuhi wamerudi huku wasichana wao waliokuja nao hawakurudi.
Hakika ni wazi katika sentensi hizi kuwa zimeundwa na sentensi/vishazi changamani tu. Sentensi hizi zinazounda sentensi ambatani ni changamani kwani zimeundwa na vishazi virejeshi.
d) Muundo wa sentensi au vishazi visivyo na kiunganishi.
- Mwambie aondoke.
- Waite warudi.
- Wafuate uwaite.
Hizi nazo ni sentensi ambatani. Ni ambatani kwa sababu zimeundwa na sentensi sahili zenye virai-vitenzi vyenye kusimama kama sentensi sahili.
e) Muundo wa sentensi zilizounganishwa na koma/mkato (,).
- Mwalimu anafundisha, wanafunzi wanaandika.
- Wavulani ni watundu sana, wasichana ni wapole kupitiliza.
- Waandishi wa habari ni makasuku, wasanii ni watambaji.
Sentensi hizi ni ambatani zisizo na viunganishi vya maneno bali zimeunganishwa na alama ya koma au alama ya mkato.
3. Sentensi changamani
Sentensi changamani ni sentensi ambazo zina muundo wa kishazi tegemezi na kishazi huru. Ni sentensi ambazo zina mchanganyiko wa vishazi viwili tofauti. Wanasarufi wanasema ya kwamba sentensi ya namna hii angalau iwe na kishazi tegemezi kimoja na kisha huru kimoja. Kishazi tegemezi huhitaji kishazi huru ili kukamilika hasa kimaana. Tazama mifano yake hapa chini.
a. Kijana tuliyekutana naye mjini alikuwa mwalimu wetu.
b. Mtu alinunua kitabu kilichoandikwa na Mbaabu.
c. Aliporudi nyumbani alitukuta tumelala.
d. Kagero ambaye nilimfundisha amemaliza masomo yake.
e. Kwa kuwa hapendi nyama mpikie samaki n.k.
Sentensi hizi zimesheheni vishazi tegemezi na vishazi huru vinavyokamilisha vishazi tegemezi. Izingatiwe kuwa sio sheria kwa sentensi changamani kuwa na kishazi tegemezi kimoja tu; bali inaweza kuwa na zaidi ya kishazi-tegemezi kimoja. Ituatayo ni miundo ya sentensi changamani:
a) Muundo wa vishazi virejeshi.
Muundo huu ni ule ambao kipashio kikubwa kama kishazi hubebwa na kipashio kidogo kama kirai. Muundo huu ni ule ambao kirai-nomino hubeba kishazi kirejeshi (Massamba et al, 2012). Mfano:
- Kuku wetu tuliyemchinja kwenye sherehe nyama yake ilikuwa tamu sana.
- Maisha yaliyobora hayana vurugu nyingi.
- Binti aliyekuwa amekuja kututembelea jana anaitwa Stella.
- Nilipokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo kule chuoni nilisingiziwa kuiba simu ya mwalimu wa shule ya msingi.
Sentensi hizi kwa sehemu kubwa zimeundwa na vishazi virejeshi, hasa katika sehemu ya virai-nomono.
b) Muundo wa vishazi vielezi.
Katika muundo huu, sehemu kubwa ya sentensi hujikita katika vishazi vielezi ambavyo hueleza hali ya vitenzi katika vishazi huru (Massamba et al, 2012). Kwa mfano;
- Alipokuwa mtoto alimpenda sana kaka yake.
- Akifaulu mtihani wake tutampongeza sana.
- Kwa sababu anapenda sana kuimba mpe gitaa.
- Tulitoka nyumbani asubuhi tukatembea kweli kweli.
Sentensi hizi zinaonesha kuwa zina vishazi vinavyoto maelezo zaidi kuhusu virai-vitenzi.
4. Sentensi shurutia
Hii ni aina ya sentensi ambazo zinakuwa zimeundwa na vishazi tegemezi tu. Huwa na utegemezi wa jambo moja kutegemea jambo lingine ili liweze kukamili. Huwa ni sentensi zente utegemezi wa kukamilishana ndani ya muundo wake. Katika sentensi hizi, kishazi tegemezi hutegemea kishazi kingine ili jambo linalolengwa likamilike. Mfano:
a) Angekuja leo tungeondoka leo.
b) Kama wangelijua wasingelitukosea.
c) Ningelikujua ningelikukong’ota.
d) Kama angaliona uzuri wake angalimuoa.
e) Japo asingeliniomba angalichukua.
Muundo wa sentensi shurutia huwa ni muundo wa vishazi tegemezi tu, vilivyoandamana.
Uainishaji wa sentensi kimaana
Uainishaji huu wa sentensi ulitiliwa maanani na wanasarufi mapokeo. Wao walizibainisha sentensi kimaana au kiuamilifu zaidi. Hawa ni waanzilishai wa sarufi ya lugha na wanajulikana kwa umashuhuri wao wa kuzichunguza tungo kwa kuangalia zaidi maana zake. Katika uanishaji huu, aina za sentensi zifuatazo zinabainika;
1) Sentensi taarifu
Hizi ni aina ya sentensi zenye kutoa taarifa fulani kuhusu kitu, mtu au jambo lolote. Mifano yake ni kama hii:
a. Ngedele amekula mahindi yangu.
b. Mjomba ameaga dunia leo.
c. Masuka ni mwnafunzi wa chuo cha ualimu Katoke.
d. Mwalimu ametuambia tusome kwa bidii ili tushinde mtihani.
e. Mboga za majani huongeza vitamini mwilini.
Sentensi hizi, uamilifu wake uko katika kujuza mambo fulani. Yaani zinatoa taarifa mbalimbali kama zinavyojidhuhirisha.
2) Sentensi ulizi (?).
Hizi ni sentensi zenye kudokeza jambo lenye kuhitaji majibu. Ni sentensi zenye kuuliza maswali yatarajiayo majibu. Huwa zina pengo katika sehemu yake ya taarifa (Habwe na Karanja, 2003:142). Ifuatayo ni mifano ya sentensi ulizi:
a. Nimekwambia ufanye nini?
b. Nyanya yako anaitwa nani?
c. Wewe umeruhusiwa na nani kugawa dafrati langu?
d. Kipi kikusikitishacho?
e. Kwa nini hukwenda kumsalimu mama yako?
Sentensi hiizi zinahitaji upande wa pili ili ziweze kupata kile kinachotarajiwa kujibiwa. Hivyo ni tungo zenye kuuliza na kutaka majibu.
3) Sentensi agizi.
Sentensi hizi hutoa maagizo yenye kuhitaji kutimizwa. Humwagiza msikilizaji kutenda kitendo fulani. Tazama mifano ifuatayo:
a. Leta hiyo kalamu!
b. Kamwite Pelanya aje hapa!
c. Fanya zoezi hili kabla ya saa nne na nusu!
d. Nenda nyumbani kwenu!
e. Zunguka uwanja mzima mara kumi!
Ukizichunguza hizi sentensi hizi, utagundua hali fulani ya uagizi ambayo msikilizaji anapaswa kutimiza.
4) Sentensi mshangao (!)
Hizi ni sentensi ambazo huonesha mshangao kwa tukio fulani, na huwa na alama ya mshangao (!). Katika wakati mwingine, sentensi hizi huitwa sentensi tashtiti zenye kuuliza maswali ambayo majibu yake hufahamika. Mfano wa sentensi hizi ni kama:
a) Aah, kumbe ni wewe!
b) Ati umeolewa?!
c) Ee, Mungu wangu!
d) Na wewe unajua kucheza?!
e) Wasalalee, umemwona amerudi akiwa njiti! n.k.

ALCHERAUS MUSHUMBWA, 2018
Shairi natunga
Nami natunga shairi, yamoyoni kuyasema
Kweli ni vema kukiri,bayana ni jambo jema
Mungu wala si bakari,waja hujalia mema
Kayasema sulutani manenowe ni sheria.

Heri njiwa kununua,kuliko  wale watumwa
Bora kazi kuibua,wao mbele kusukumwa
Njaazo kusisimua,zingoje tunda kuchumwa
Kayasema sulutani,manenowe ni sheria.

Mara ya mia elimu,bure na ipatikane
Shida zao hao walimu,subiri tutulizane
Wakinena mahasimu,wamejambatuuchune
Kayasema sulutani,manenowe ni sheria

Zinjengwe kwanza njia, wajenzi leo wasile
Punda afe nasikia,zege katu lisilale
Wengi wanamlilia,tabu zao tangu kale
Kayasema sulutani,manenowe ni sheria.

Watumwa mlo wakila,Kazi nzuriwatachapa
Na sulutani kalala,hataki haki kuwapa
Kuwanyima wao kula,sote twatapatapa
Kayasema sulutani,manenowe ni sheria.

Shime nawausieni,enyi Watumwa wa heri
Kazi daima chapeni,kudai sio hatari
Sauti zenu pazeni,madai  yawe habari
Kayasema sulutani,manenowe ni sheria.

©sir manyuka
DHANA YA SARUFI YA KISWAHILI
na
Alcheraus R. Mushumbwa, 2017

Maana ya Sarufi
Lugha za binadamu huwa na mpangilio maalumu wa sauti za binadamu zilizokubaliwa na wanajamii fulani ili zitumike katika mawasiliano yao - wao kwa wao, kwa kufuata utaratibu maalumu. Dhana ya lugha kwa jumla inajidhihirisha bayanikatika mhimili wa mawasiliano; kwa maana kuwa, lugha ni chombo cha kimawasiliano kati ya binadamu na binadamu au jamii na jamii katika eneo fulani kama kabila au taifa, na kadhalika. Hivyo basi, jukumu la kutimiza dhima ya kukidhi haja ya mawasiliano katika jamii kupitia lugha haliwezi kutimia kama chombo hicho (lugha) hakijaundiwa utaratibu maalumu. Utaratibu huo huundwa na wanajamii kwa lengo la kuweka kaida au sheria zinazopaswa kuwaongoza watumiaji wa lugha hiyo ili kuweza kufikisha ujumbe unaoeleweka. Utaratibu huo ndiyo unaoitwa sarufi ya lugha fulani.

Sarufi ni nini?
Kujibu swali la sarufi ni nini, kunaweza kuchukua mamia ya miaka na rundo la maelezo yaliyojazwa kwenye vitabu pamoja na vyanzo mbalimbali vya maarifa lakini bado majibu yake yasifikie kikomo. Hii ni kwa sababu sarufi inahusu lugha; na lugha yenyewe huendelea kupanuka kutoka vizazi hadi vizazi, na hivyo, kuifanya sarufi nayo isiwe na kikomo cha kuifafanua. Maelezo haya yanaelekeza wazi kuwa sarufi ni taaluma pana yenye mambo si haba kuhusu lugha. Kwa maana hiyo, kitabu hiki hakiwezi kueleza kila kitu kuhusu sarufi bali kinagusia baadhi ya vipengele vya sarufi ya Kiswahili ambavyo hupendekezwa kufundishwa katika elimu ya upili wa chini hasa kwa shule za Tanzania. Mara baada ya maelezo haya mafupi ya utangulizi ni muda mwafaka wa kujaribu kutazama majibu ya swali hili. Baadhi ya wataalamu wa isimu (sarufi) wamejaribu kujibu nini maana ya sarufi kama ifuatavyo:
Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (1988:28), wanaeleza sarufi kuwa ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matamshi, maumbo, miundo na maana katika lugha. Wanaendelea kufafanua kuwa taratibu na kanuni hizi humwezesha mzawa au mtumiaji yeyote wa lugha: 1) kutoa tungo sahihi na zinazoeleweka, 2) kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetumia lugha hiyo.Katika Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK, 2015: 912), sarufi imeelezwa kuwa ni tawi la isimu ya lugha linalojishughulisha na fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia. Kwa ufupi, maana ya isimu katika lugha ni taaluma inayochunguza na kuchambua mfumo na muundo wa lugha za binadamu. Fonolojia ni sarufi matamshi inayohusika na uchunguzi pamoja na uchambuzi wa utamkaji sauti za binadamukatika lugha husika; na, jinsi sauti hizo zinavyotamkwa na mahali zinapotamkwa sambamba na vipashio vyake. Mofolojia ni sarufi maumbo inayojihusisha na maumbo ya maneno katika lugha. Sintaksia ni sarufi miundo inayochunguza miundo na mpangilio wa maneno katika lugha; nayo, semantiki ni sarufi maana ambayo huchunguza maana katika lugha za binadamu. Sambamba na maelezo ya Taasisi ya Ukuzaji Mitaala na Kamusi Kuu ya Kiswahili,Brinton(2000:8), naye anasema kuwa “sarufi katika taaluma ya lugha, hutumika kurejea kanuni au miongozo, ambayo hutawala lugha.” Kwa maana hiyo, na kwa mtazamo huu, sarufi ni kanuni, sheria au taratibu ambazo lugha husika hujipambanua. Kanuni hizo ndizo huongoza matumizi ya lugha. Kwa jumla, sarufi inaweza kufasiliwa kuwa ni kanuni au taratibu zinazotawala na kuongoza matumizi ya lugha husika. Kanuni hizo huwaongoza watumiaji wa lugha hiyo katika kutumia lugha kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutunga na kuunda tungo sahihi na zinazokubalika katika mfumo wa lugha ya jamii fulani.
Sarufi ya Kiswahili ni nini?
Kama lilivyojibiwa swali la sarufi ni nini, vivyo hivyo, ndivyo hata swali la Sarufi ya Kiswahili ni nini linavyojibiwa, ikimaanishwa kuwa majibu yake yanatokana na msingi wa kurejea wataalamu waliojishughulisha na sarufi ya Kiswahili. Kama ilivyorejelewa mwanzo katika kujibu swali la maana ya sarufi, vilevile Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (1988:28) wanasema kuwa Sarufi ya Kiswahili ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazotawala matumizi sahihi ya matamshi ya maneno, maumbo ya maneno, miundo ya tungo na maana ya miundo ya Kiswahili. Ni mfumo wa taratibu zinazomwezesha mzungumzaji wa lugha ya Kiswahili kutoa tungo sahihi za Kiswahili na pia zinazomwezesha mtu yeyote anayezungumza Kiswahili kuelewa tungo zinazotolewa na mtu mwingine anayetumia lugha ya Kiswahili. Waaidha, Masebo na Nyangwine (2010:72) wanasema kwamba Sarufi ya Kiswahili ni kanuni zinazotawala maumbo, matamshi, miundo na maana katika lugha ya Kiswahili. Hivyo, sarufi ya Kiswahili, ni sarufi ambayo hujikita katika lugha ya Kiswahili. Ni taratibu na miongozo ya utumiaji wa lugha ya Kiswahili. Kutokana na fasili ya sarufi ya Kiswahili, ni wazi kabisa kuwa sarufi ya lugha ya Kiswahili huwasaidia wazungumzaji wa lugha hii kutambua miundo sahihi ya sentensi wanazozitunga na maneno wanayoyaunda; kuelewa tungo zinazotungwa na watumiaji wengine wa lugha ya Kiswahili. Sarufi ya Kiswahili imegawanyika katika viwango (tanzu) vikuu vinne ambavyo ni: sarufi matamshi, sarufi maumbo, sarufi miundo na sarufi maana.

Viwango vya Sarufi ya Kiswahili
Neno ‘viwango’ hapa limetumika badala ya tanzu au matawi, au vipengele. Kwa hiyo, viwango vya sarufi ya Kiswahili ni vipengele au tanzu au matawi ambayo sarufi ya Kiswahili imegawanyika. Kama ilivyodokezwa, viwango hivi vipo vinne ambavyo ni:

Sarufi Matamshi
Kwa mujibu wa Kadeghe (2012:80), sarufi matamshi huchambua vitamkwa (fonimu) vya lugha inayohusika, ikionesha namna na mahali kila kitamkwa kinapotamkwa. Neno ‘vitamkwa’ (kikiwa kimoja ni ‘kitamkwa[1]’) limetumika badala au kumaanisha sauti zinazotamkwa katika lugha fulani.Naye Matinde (2012:58), anasema sarufi matamshi ina wajibu wa kuchunguza na kufafanua sauti za lugha na uamilifu wake katika mfumo mahususi. Anachokisema Matinde hapa, ni kwamba kazi kubwa ya sarufi matamshi ni kuchunguza na kutoa ufafanuzi kuhusu utendaji kazi wa sauti za binadamu katika lugha maalumu. Hivyo basi, sarufi matamshi ni kiwango au kipengele cha sarufi kinachohusika na uchunguzi pamoja na uchambuzi wa sauti za lugha mahususi. Sauti za lugha mahususi ina maana ya kuwa ni sauti za lugha fulani kama Kiswahili, Kingoni, Kisukuma, Kinyarwanda, Kichina n.k. Zinakuwa sauti maalumu au mahususi pale zinapobainishwa kuwa ni sauti za lugha fulani kama mifano iliyotajwa hapa. Sarufi matamshi ya Kiswahili huchunguza sauti za binadamu na utendaji kazi wake katika lugha ya Kiswahili – yaani, huchunguza uamilifu wa sauti za lugha ya Kiswahili. Aidha, inachunguza na kubainisha sifa za sauti, uamilifu wake na jinsi sauti hizo zinavyotamkwa na kuambatana katika kuunda vipashio vikubwa zaidi ya fonimu; huchunguza namna na mahali sauti hutamkiwa. Pia, Sarufi matamshi hujulikana kama fonolojia au umbo-sauti.[2]

Sarufi Maumbo
Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (KSIL, 1990:40) inatoa fasili ya sarufi maumbo kuwa ni “tawi la isimu (maana ya isimu imefafanuliwa, rejea maana ya sarufi) ambalo huchunguza maneno na aina za maneno.” Hiki ni kiwango au kipengelecha sarufi ambacho hujikita katika uchunguzi wa maumbo ya maneno kwa kuzingatia uchunguzi wa miundo (jinsi manenoyanavyoundwa) ya maneno, makundi ya maneno na uhusiano wa maneno pamoja na taratibu za uundaji wa maneno. Sarufi maumbo ya Kiswahili huchunguza na kuchambua maumbo ya maneno ya Kiswahili, na namna maumbo hayo yanavyotumika kuunda maneno katika lugha ya Kiswahili pamoja na maana au dhana zinazowakilishwa na maumbo hayo. Tawi hili la sarufi, hushughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipashio vya kimaumbo kama mofu na alomofu zake, viambishi, mzizi, shina pamoja na uamilifu wa vipashio hivyo sambamba na mofimu za vipashio hivyo (maana zinazobebwa na vipashio vilivyotajwa). Huchunguza pia uainishaji wa aina za maneno kwa kuzingatia kigezo cha kimaumbo, kimuundo na kimaana.

Sarufi Miundo
Hiki ni kiwango cha sarufi kinachojulikana pia kama sintaksia. Massamba na wenzie (2012:1) wanaeleza kuwa sarufi miundo ni utanzu wa sarufi unaojishughulisha na uchanganuzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Nao TUKI (1990) wanafasili sarufi miundo kuwa ni tawi la isimu (sarufi) linaloshughulikia uchanganuzi wa mpangilio na uhusiano wa vipashio katika kila sentensi. Fasili za wataalam hawa zikichunguzwa kwa umakini zinabainisha kitu kimoja au kilekile. Hii ni wazi kuwa sarufi miundo ni sarufi inayoshughulikia miundo ya tungo katika lugha. Huchunguza mpangilio wa tungo katika lugha ya binadamu na jinsi mpangilio huo unavyoweza kudokeza maana au dhana iliyolengwa na iliyo sahihi.Sarufi miundo ya Kiswahili hujikita kwenye kuchunguza na kuchambua miundo ya tungo za Kiswahili. Kwa maana hiyo, sarufi miundo si kitu kingine bali ni kipengele cha sarufi chenye kujikita katika uchunguzi, uchambuzi na ufafanuzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Fauka ya hayo, katika tawi hili la sarufi kinachochunguzwa ni zile sheria au kanuni ambazo ni lazima zifuatwe katika kupanga maneno ya lugha katika mfuatano kwa namna ambayo inafanya maneno hayo kuleta maana inayokubalika na kueleweka katika lugha fulani. Huchunguza tungo kama neno inavyoweza kuungana na tungo neno kuunda tungo kirai au tungo kishazi hadi sentensi sanjari na kuchunguza viambajengo vinavyounda tungo hizi.

Sarufi Maana (Semantiki)
Sarufi maana ya Kiswahili, kwa jina lingine hujulikana kama semantiki au umbo-sauti.[3] Wanaisimu Habwe na Karanja (2004:201) wanafafanua sarufi maana kuwa ni utanzu wa sarufi unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu. Vilevile, Mekacha (2011:13) anaeleza kuwa semantiki ni taaluma inayochanganua na kufafanua miundo na mifumo ya maana na kipashio chake cha msingi katika uchanganuzi ni leksimu, umbo lenye maana moja. Kwa maana hiyo basi, ni dhahiri kuwa sarufi maana ni kipengele cha sarufi kinachochunguza na kuchambua maana katika lugha za binadamu. Sarufi maana ya Kiswahili huchunguza na kuchambua maana zinazokuwa zimebebwa na tungo katika lugha ya Kiswahili. Maana zinazochunguzwa kwenye kiwango hiki cha sarufi ni zile maana za maneno, vifungu vya maneno (kirai na kishazi) na sentensi. Hapa ndipo wanasarufi (isimu) huchunguza na kuchambua nadharia mbalimbali zinazofasili maana, aina za maana, jinsi ufasili wa watumiaji wa lugha huathiri maana katika lugha. Kiwango hiki kimekua na kutanuka zaidi hadi kufikia hatua ya kuzaa kipengele kingine kinachoitwa pragmatiki. Pragmatiki ni isimu inayochunguza maana za usemi katika muktadha maalumu. Huchunguza jinsi maana zinavyofasiliwa na wazungumzaji kulingana na mazingira ambamo mazungumzo hayo hutokea. Japo kumekuwepo na mtazamo kwa baadhi ya wanaisimu kuipa hadhi ya upekee kama utanzu wa isimu unaojitosheleza lakini mama mzazi wa pragmatiki kama taaluma ya maana ni isimu maana (sarufi maana).
Hadi kufika hapa, kwa kiasi fulani sarufi imeelezwa japo si kwa kirefu ila ufafanuzi huu unatosha kutoa mwanga na uelewa wa dhana ya sarufi na vipengele vyake kwa jumla.

Maswali
(a)  Eleza maana ya sarufi.
(b)  Fafanua kwa mifano sarufi ya Kiswahili maana yake ni nini?.
(c)   Taja na ueleze kwa ufupi tanzu tano za sarufi ya Kiswahili

MAREJEO
BAKITA,Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK), Dar es Salaam: Longhorn Publishers Limited,
               2015.
Brinton, Laurel J, The Structure of Modern English: A linguistic Introduction, Amsterdam:
                      John Benjamin Publishing Company, 2000.
Habwe, John na Peter Karanja, Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Kenya: Phoenix Publishers,
              2004.
Kadeghe, Michael, Kiswahili kwa Shule za Sekondari Tanzania Kidato cha Kwanza,
                 Toleo la 3,Dar es Salaam: Jamana Printers Limited, 2012.
Kihore, Y. M., D. P. B. Massamba na Y. P. Msanjila, Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu
                (SAMAKISA) Sekondari na Vyuo, Chapa ya 6, Dar es Salaam: TUKI, 2012.
Mhilu, Greyson na Masebo J. A, Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha Tatu, Dar es
            Salaam: Nyambari Nyangwine Publishers, 2010.
Matinde, Riro S, Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia, Mwanza: Serengeti Educational
                Publishers (T) Ltd, 2013.
Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Kiswahili Sekondari, Dar es Salaam: Kitabu Commercial Ltd,
           1988.
TUKI,Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha.Dar es Salaam: Eductational Publishers and
             Distributors Ltd, 1990


[1]Kamusi Kuu ya Kiswahili inatoa fasili ya neno ‘kitamkwa’ kuwa ni kipande sauti katika mfumo wa lugha chenye sifa bainifu kis.: fonimu.
[2]Rejea Y.M.Kihore na wenzake (2012:2)
[3]Wataalamu wa Isimu,Massamba na wenzie (2012:30) na Kihore na wenzie (2012: 3) wanatumia istilahi ‘umbo-maana’ kurejelea dhana ya sarufi maana (semantiki).

UPATANISHO WA KISARUFI KATIKA KISWAHILI

ALCHERAUS R. MUSHUMBWA, 2018

1. Maana ya upatanisho wa Kisarufi
Kwa mujibu wa BAKITA (2015:1107), upatanisho wa kisarufi ni kukubaliana kisarufi kunakojitokeza kati ya nomino kiima na kitenzi au na kivumishi kunakobainishwa na viambishi. Kwa mwongozo huo, tunafasili patanisho wa kisarufi kuwa ni kukubaliana kisarufi kunakojitokeza kati ya nomino kiima na kitenzi; au, na kivumishi kunakobainishwa na viambishi. Kukubaliana huku huwa kunahusisha nomino mtenda au mtendwa, kiwakilishi, kivumishi na kitenzi kwenye mpangilio sahihi wa sentensi za Kiswahili. Hii ina maana kuwa viambishi (awali) vinavyoambikwa kwenye kivumishi au kitenzi katika sentensi huzingatia aina ya nomino mtenda au kiwakilishi chake au nomino mtendwa kwa sababu nomino mtenda au mtendwa kwenye tungo za Kiswahili huwa ndiyo mhusika anayetolewa taarifa katika tungo husika. Viambishi vya upatanishi wa kisarufi katika Kiswahili sanifu huteuliwa kulingana na aina na pia kundi (ngeli) la nomino mtenda au mtendwa inayoarifiwa. Lengo la upatanisho wa kisarufi ni kuleta maana sahihi na yenye mantiki kwa wazungumzaji.

Utokeaji wa Upatanishi wa Kisarufi
Upatanishi wa kisarufi katika tungo za lugha ya Kiswahili hutokea kwenye vipashio mbalimbali vinavyounda tungo husika kulingana na taratibu za kisarufi (Mhilu na Masebo, 2010:1-2).
a)      Nomino na Kivumishi (N+V)
Mizizi ya vivumishi vya Kiswahili huchukua viambishi vya upatanisho kulingana na nomino inayovumishwa ipo katika kundi lipi kwa kuzingatia umoja na wingi ili kuleta uafikiano. Kwa mfano:
1.      Mtu mwema (umoja)/ Watu wema (wingi)
Mbwa mzuri (umoja)/ Mbwa wazuri (wingi)
2.      Kitabu changu (umoja)/ Vitabu vyangu (wingi)
Kiti kirefu (umoja)/ Viti virefu (wingi).

b)      Nomino na kitenzi (N+T)
Upatanisho huu unahusisha nomino mtenda katika tungo pamoja na viambishi awali vinavyoambikwa kwenye mzizi wa kitenzi ili kuleta ukubalifu wa tungo kimuundo. Kitenzi (mzizi) hulazimika kuchukua kiambishi awali kinachoendana na nomino mtenda kwenye tungo ambapo kiambishi hicho hutambulika kulingana na nomino iko kwenye kundi lipi la majina katika umoja na wingi. Kwa mfano:
1.      Uovu umezidi mtaani kwetu (umoja)/Maovu yamezidi mtaani kwetu (wingi)
2.      Mto umekauka (umoja)/Mito imekauka (wingi)



c)      Nomino, kivumishi na kitenzi (N+V+T)
Katika mpangilio huu wa tungo, upatanisho wake huwa ni ukubalifu wa mpangilio sahihi wa vipashio (nomino mtenda+kivumishi+kitenzi) ambapo kivumishi (mzizi wake), na kitenzi (mzizi wake) hukubali kuchukua viambishi awali vinavyoitabulisha nomino mtenda kwenye tungo hiyo. Upatanisho huu nao hufuata utaratibu wa kuzingatia aina ya nomino na kundi lake inamojumuishwa katika makundi ya majina. Kwa mfano:
1.      (a) Ukuta ule umebomoka (umoja)/Kuta zile zimebomoka (wingi)
(b) Ukuta wangu umebomoka (umoja)/Kuta zangu zimebomoka (wingi)
(c) Ukuta mzuri/mrefu umebomoka (umoja)/Kuta nzuri /ndefu zimebomoka (wingi)
2.      Kucheza kwake kunachosha.

d)     Kitenzi na nomino mtendwa (T+N-mtendwa)
Hapa upatanisho hutokea pale kitenzi kinapotangulia jina au nomino ambayo ndiyo huwa imeathirika na tendo. Kiambishi cha upatanisho wa mtendwa huwa katika kitenzi na kiambishi hicho huwa ndicho kiwakilishi cha nomino hiyo kwa utaratibu wa kuzingatia kundi ambalo nomino hiyo imo. Kwa mfano:
1.      Umemtuma Juma dukani? (umoja)/Umewaita watoto wale? (wingi)
2.      Ameikata kamba yangu (umoja/Amezikata kamba zangu (wingi)

e)      Kiwakilishi na Kivumishi (W+V)
Kiwakilishi ni neno linalochukua nafasi ya nomino au jina katika sentensi. Hivyo, bila kuwepo nomino basi nafasi yake inachukuliwa na kiwakilishi. Upatanishi wa kisarufi pia huvikumba viwakilishi vya Kiswahili pale vinapofanya kazi ya nomino mtenda au mtendwa katika tungo. Kwa hiyo, upatanishi wa kiwalikishi na kivumishi ni pale kivumishi (mzizi wake) kinapokubali kuchukua kiambishi awali kinachowakilisha kiwakilishi ili kuleta ukubalifu wa kimuundo kwenye sentensi. Kwa mfano:
1.      Mimi mfupi sana (umoja)/Sisi wafupi sana (wingi)
Huyu mnene kabisa (umoja)/Hawa wanene kabisa (wingi)
2.      Hiki chembamba (umoja)/Hivi vyembamba (wingi)
Kile kifupi (umoja)/Vile vifupi (wingi)

f)       Kiwakilishi na kitenzi (W+T)
Kitenzi kinachoandamana na kiwakilishi kwenye tungo, mzizi wake huambikwa kiambishi awali kipatanishi kinachoiwakilisha nomino inayowakilishwa na kiwakilishi hicho ili kuleta uafikiano wa vipashio hivyo kwenye tungo. Ifuatayo ni mifano ya upatanisho wa kisarufi kati ya Kiwakilishi na Kitenzi:
1.      Hili limeharibika (umoja)/Haya yameharibika (wingi)
Zuri limeharibika (umoja)/Mazuri yameharibika (wingi)
2.      Ule umekatwa (umoja)/Ile imekatwa (wingi)
g)      Kiwakilishi, kivumishi na kitenzi (W+V+T)
Katika upatanisho huu, kivumishi na kitenzi vinavyoandamana na kiwakilishi ili kuunda tungo, hulazimika kupokea viambishi awali vya upatanishi vinavyowakilisha nomino mtenda inayowakilishwa na kiwakilishi kilicho katika tungo husika ili kuleta uafikiano au ukubalifu sawia. Kwa mfano:
1.      Langu lile limepotea (umoja)/Yetu yale yamepotea (wingi)
2.      Kimoja kidogo kimenunuliwa (umoja)/Vingi vidogo vimenunuliwa (wingi)

h)      Kitenzi na kiwakilishi (T+W)
Hapa, tungo huwa inahusisha kitenzi na kiwakilishi ambapo kitenzi hutangulia kiwakilishi cha nomino mtendwa. Upatanisho wake huwa ni pale ambapo kitenzi hubeba kiambishi cha upatanisho wa kisarufi ambacho huiwakilisha nomino mtendwa inayowakilishwa na kiwakilishi. Kawa hiyo, ili tungo ilete mantiki na ukubalifu sahihi inabidi kitenzi kikubali kupokea kiambishi cha upatanisho kinachowakilisha kiwakilishi cha nomino mtendwa. Kwa mfano:
1.      Amepigwa yeye mwenyewe/Wamepigwa wao wenyewe
Nimetumwa mimi/Tumetumwa sisi
2.      Kimenunuliwa kirefu/Vimenunuliwa virefu
Hadi kufikia hapa, angalau kwa kiasi, dhana ya upatanishi wa kisarufi katika lugha ya Kiswahili imeelezewa na kupata picha halisi ya jinsi upatanishi wa kisarufi huchukua nafasi kwenye lugha ya Kiswahili. Aidha, kinachoweza kuelezwa kwa ufupi ni kwamba kinachoongoza kanuni ya upatanishi wa kisarufi ni mlengwa mkuu katika tungo – yaani, nomino mtenda au mtendwa kama ilivyodhihirishwa kwenye ufafanuzi na mifano yake. Kanuni inayoongoza upatanishi wa kisarufi inasema kuwa nomino mtenda au mtendwa pamoja na kiwalikishi chake itawakilishwa katika kivumishi au kitenzi kinachoandamana nayo kwenye tungo kwa umbo au maumbo (viambishi) yanayoitambulisha nomino hiyo kulingana na umilikwaji wake kwenye kundi au ngeli za majina.” Kwa maana hii basi, kinachofanya utambuzi wa kupachika viambishi vitakavyoleta upatanishi kwenye tungo ni yale maumbo yanayoiwakilisha nomino husika kwenye ngeli au kundi inamomilikiwa. Kanuni hii hutambuliwa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili kwenye akili zao pale wanapokuwa wanazungumza au kuandika kwa lengo la kuwasiliana. 

MAREJEO
BAKITA,Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK), Dar es Salaam: Longhorn Publishers Limited,
               2015.
Mhilu, Greyson na Masebo J. A, Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha Tatu, Dar es
            Salaam: Nyambari Nyangwine Publishers, 2010.
Mlyauki, Justa, E. mulashani na D. Ndilime, KiswahiliKitukuzwe 3, Malaysia: Pearson
              Education Limited, 2009.


Copyright © 2012 JUKWAA LA KISWAHILI